Mwana FA: Rais Samia kuiwezesha Simba

DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, amepokea maagizo maalum kutoka kwa Rais, Samia Suluhu Hassan, kuzungumza na uongozi wa Klabu ya Simba SC.
Akiwa na dhamira ya kuhakikisha Tanzania inaandika historia kwenye medani ya soka Afrika, Mwana FA amesema Rais Samia ameelekeza serikali kuwasaidia Simba kwa kila njia wanayoweza kuelekea mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF dhidi ya RS Berkane ya Morocco
“Tayari Rais Samia ametuelekeza kuhakikisha hatuwei kikwazo chochote kwa Simba. Hatuwezi kusema tutawasaidia kwa lipi hasa mpaka tukutane nao na kusikia mahitaji yao. Lakini dhamira ya serikali ni moja kuhakikisha Simba wanapata kila msaada unaohitajika kushinda ubingwa wa CAF,” amesema Mwana FA.
Simba wanatarajia kusafiri kuelekea Morocco kwa ajili ya mechi ya kwanza ya fainali itakayopigwa Mei 17, huku mchezo wa marudiano ukitarajiwa kuchezwa Mei 25 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mwana FA ameeleza kuwa serikali imeridhishwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Simba kufikia hatua hii ya kihistoria. Ameongeza kuwa kile kilichofanywa katika hatua ya nusu fainali dhidi ya Stellabosch FC, ambapo serikali iliwezesha usafiri na malazi kitafanyika tena kwa nguvu zaidi katika fainali.
“Kumbuka katika nusu fainali tulisaidia Simba wamende Afrika Kusini kwa ajili ya marudiano dhidi ya Stellabosch. Matokeo yalikuwa mazuri na sasa tuna nafasi ya kufanya historia. Fainali ya marudiano itapigwa nyumbani, na hilo linamaanisha kombe linaweza kuinuliwa hapa nchini,” ameongeza.