Nyumbani

Mukwala:Tunauwezo wa kupindua meza Zanzibar

DAR ES SALAAM:KATIKA harakati za kuandika historia mpya kwenye soka la Tanzania, mshambuliaji hatari wa Simba, Steven Mukwala, ameweka bayana kuwa kikosi chao kiko tayari kwa mapambano na kinaamini kina uwezo wa kugeuza matokeo katika mchezo wa marudiano dhidi ya RS Berkane ya Morocco.

Simba inakabiliwa na kibarua kizito Jumapili, Mei 25, kwenye uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, ambapo wanapaswa kushinda kwa mabao 3-0 ili kujihakikishia taji la Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kupoteza kwa mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza nchini Morocco.

Mukwala amesema licha ya changamoto ya mabao mawili waliyofungwa, morali ya timu iko juu na kila mchezaji anafahamu uzito wa mchezo huo.

“Tunajua tupo nyuma kwa mabao mawili, kazi kubwa lakini siyo jambo lisilowezekana. Tunasahihisha makosa na maandalizi yanaendelea vizuri. Tuko tayari kucheza kokote  iwe Benjamin Mkapa au Zanzibar, kote ni nyumbani kwetu,” amesema.

Mukwala ameongeza kuwa benchi la ufundi limekuwa makini kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza katika mchezo wa kwanza ili kuhakikisha timu inakuwa bora zaidi kwenye marudiano.

Kwa sasa macho yote ya wanasimba na wapenda soka wa Tanzania kwa ujumla, yako Zanzibar, ambapo historia inaandikwa, matumaini yakiwa kwamba Simba wataweza kuleta taji hilo nyumbani kwa mara ya kwanza

Related Articles

Back to top button