Muhogo Mchungu Ampa Tano Rais Samia

DAR ES SALAAM:MWIGIZAJI mkongwe nchini, Abdallah Mkumbila maarufu kama Muhogo Mchungu, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake katika kuunga mkono sekta mbalimbali, ikiwemo burudani na michezo, na kuhakikisha zinapiga hatua za maendeleo.
Muhogo Mchungu ameliambia SpotiLeo kuwa kiongozi huyo anastahili heshima kwa kuwa ni mwepesi wa kushughulikia changamoto za makundi mbalimbali ya kijamii.
“Tumempata Rais shupavu, mvumilivu na mstahimilivu. Matatizo yote amekuwa akiyatafutia ufumbuzi. Ni mtu mwenye huruma kwa sababu ameangalia makundi yote na kuyagusa kwa namna mbalimbali,” amesema.
Amesema anashangazwa na baadhi ya watu ambao, licha ya kusaidiwa, wanashindwa kutoa shukrani na badala yake hugeuza msaada huo kwa kutukana.
“Kuna wizi wa fadhila na uchoyo wa fadhila. Mtu anafadhiliwa lakini hatoi shukrani kwa kile alichofanyiwa. Binadamu tuna hila kama kuku,” amesema.