Msuva arudi nyumbani kusaka vipaji

DAR ES SALAAM: NYOTA wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Simon Msuva amesaini mkataba rasmi na Kampuni ya TBL kupitia bia ya Safari Lager kwenye mchakato wa mashindano maalum ya kuibua vipaji vya vijana nchini.
Kupitia mkataba wa makubaliano, Msuva atakuwa sehemu ya programu hiyo kwa lengo la kuwasaidia vijana wanaochipukia kupata nafasi ya kuonekana na kuendeleza vipaji vyao.
Msuva, ambaye kwa sasa anacheza soka la kulipwa katika klabu ya Al Talaba SC ya Iraq, amesema ameamua kutumia mapumziko yake kwa kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo la kusaka vipaji akishirikiana na makocha pamoja na maskauti wa mashindano hayo.
Msuva amesema:“Jumamosi, Mei 31, nitakuwepo Uwanja wa Nyamagana, Mwanza, nikiwa na kocha Sakilojo Chambua kushiriki kwenye mashindano ya kutafuta vipaji. Hii ni nafasi adhimu kwangu kusaidia vijana kuonekana na kuendeleza ndoto zao.”
Msuva amesisitiza umuhimu wa vijana kutumia vyema fursa hii, akifananisha hali hiyo na kipindi chake cha ujana ambapo hakukuwa na mifumo thabiti ya kuwaibua wachezaji.
“Ninaamini vipaji vipo vingi sana mitaani, na kupitia mpango huu vitaonekana. Ukiniangalia mimi, Mbwana Samatta na wengine, kuna wengi zaidi wanaokuja nyuma yetu na taifa litanufaika nao,” amesema.
Kwa upande wake, Meneja wa bia ya Safari Lager, Pamela Kikuli, amesema Msuva ni chaguo bora kwa kuwa ana uzoefu, hadhi, na dhamira ya kweli ya kusaidia vijana.
“Kwa kipindi hiki cha mapumziko, Msuva ataungana na maskauti wengine kusaka vipaji mikoani. Jumamosi hii tunaanzia Mwanza, na tunatarajia kuona vipaji lukuki vikijitokeza,” alisema Pamela.
Mashindano ya Safari Lager yanalenga kuwa chachu ya mabadiliko kwa vijana wa Kitanzania kupitia michezo, hasa soka, kwa kuwapa jukwaa la kuonyesha uwezo wao na kuvutia macho ya makocha wa ndani na nje ya nchi.




