Mshtuko wa bega wakwamisha safari ya Changalawe

GLASGOW: NAHODHA wa Timu ya Taifa ya Ngumi ‘Faru Weusi’, Yusuf Changalawe, ameshindwa kutinga hatua ya robo fainali baada ya kupata mshtuko wa bega uliomkwamisha katika pambano lake dhidi ya Robert Okaka wa Kenya.
Katika pambano hilo la uzani wa Light Heavyweight (kg 80), Changalawe alipoteza kwa uamuzi wa pamoja wa majaji, baada ya kushindwa kucheza katika kiwango chake kutokana na majeraha ya bega yaliyompata wakati wa pambano.
Changamoto hiyo ilimlazimu kubadili mbinu zake na kushindwa kutekeleza mpango wake wa awali wa kupambana na mpinzani wake.
“Haya ni matokeo ambayo sikuyatarajia. Nilikuwa na imani kuwa mpinzani alikuwa ndani ya uwezo wangu, lakini majeraha ya bega yalinizuia kutoa kiwango changu halisi. Hata hivyo, nitaendelea kupambana na kujipanga kwa mashindano yajayo,” amesema.
Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) linampongeza Yusuf Changalawe kwa uzalendo, juhudi na mapambano aliyoyaonesha katika kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano hayo, na linaendelea kumuombea apone haraka ili arejee ulingoni akiwa na nguvu zaidi.
MWISHO




