La Liga

Modric aacha ujumbe mzito akiaga madrid

MADRID: Mkongwe na nahodha wa Real Madrid Luka Modric, amefichua kuwa ataachana na wababe hao wa Spain baada ya kumalizika kwa kampeni yao ya Kombe la Dunia la Vilabu la FIFA linalotarajia kuanza Juni 15 mwaka huu huu.

Kiungo huyo wa kati wa Croatia mwenye umri wa miaka 39, pia ni mshindi wa Ballon d’Or mwaka 2018 ametumia mtandao wake wa Instagram kuagana na mashabiki wa Los Blancos huku akitarajiwa kukipiga kwa mara ya mwisho kwenye dimba la Santiago Bernabeu wakati watakapoikaribisha Real Sociedad katika mchezo wa kufunga pazia la LaLiga.

Luka Modric aliandika:

“Wakati umewadia. Wakati ambao sikuwahi kutaka ufike, lakini ndio soka, na kwenye maisha kila kitu kina mwanzo na mwisho hatimaye jumamosi nitacheza mechi yangu ya mwisho Santiago Bernabeu.”

“Niliwasili hapa mwaka 2012 nikiwa na matumaini ya kuvaa jezi ya timu bora zaidi duniani na nia ya kufanya mambo makubwa, lakini sikuweza kufikiria nini kitafuata. Kuichezea Real Madrid kulibadilisha maisha yangu kama mwanasoka na kama mtu. Najivunia kuwa sehemu ya enzi yenye mafanikio zaidi ya klabu bora zaidi katika historia ya mpira wa miguu.”

“Katika miaka hii yote nimepitia mengi ya kuacha mdomo wazi, ‘comebacks’ ambazo zilionekana haziwezekani, fainali, sherehe na siku za maajabu Bernabéu… Tulishinda kila kitu na nilifurahi sana”

“Lakini zaidi ya mataji na ushindi, moyoni mwangu nimejawa mapenzi ya dhati kwa mashabiki wote wa Madrid. Kwa kweli sijui jinsi ya kuelezea uhusiano nilionao nanyi na jinsi nilivyoungwa mkono, kuheshimiwa na kupendwa nilivyohisi na kuhisi. Sitasahau kamwe kila ishara na ishara zote za upendo mlizonionesha”.

“Nondoka na moyo safi. Na nimejawa fahari, shukrani na kumbukumbu zisizoweza kusahaulika. Na hata kama baada ya Kombe la Dunia la Klabu, sitavaa tena jezi hii uwanjani, nitakuwa shabiki wa Madrid wa muda wote. Tutaonana tena. Real Madrid itakuwa nyumbani kwangu kwa maisha yote”

Tangu atue Bernabeu, Luka ameshinda mataji 28, yakiwemo sita ya Ligi ya Mabingwa na mataji manne ya LaLiga, tangu ajiunge na Real kutoka Tottenham mwaka 2012 na atakuwepo Real madrid itakapofungua kampeni ya Kombe la Dunia la Vilabu dhidi ya Al-Hilal ya Saudi Arabia Juni 18 kabla ya kuwavaa Pachuca ya Mexico na RB Salzburg ya Austria katika hatua ya makundi.

Related Articles

Back to top button