Burudani

Michezo ni njia ya kuimarisha afya, uchumi na mahusiano ya kimataifa (BMT)

DAR ES SALAAM:WATANZANIA wametakiwa kujikita zaidi katika michezo si kwa ajili ya burudani pekee bali kama njia ya kuimarisha afya ya akili, kukuza uchumi wa nchi na kujenga mahusiano ya kimataifa.

Wito huo umetolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, ambaye ameeleza kuwa michezo ni sekta yenye mchango mkubwa katika pato la taifa.

“Watanzania tuna nafasi kubwa ya kujipatia kipato kupitia michezo. Ili tufanikishe hilo, ni muhimu kujenga miili yetu na kuheshimu afya zetu kwa ujumla, hasa afya ya akili,” amesema Neema.

Ameeleza kuwa michezo husaidia kupunguza msongo wa mawazo, kujenga mwili wenye afya bora, na kuongeza ari ya kufanya kazi kwa bidii — mambo ambayo yanachangia moja kwa moja katika kukuza uchumi wa nchi.

Amesisitiza pia kuwa kwa mwanamichezo, hata kushiriki tu mashindano kunaweza kumuingizia kipato, kabla hata ya ushindi.

“Unakuta mwanamichezo anapopata nafasi ya kushiriki shindano, tayari kuna kiasi cha pesa anakipata kabla hata hajashinda. Hii inaonyesha namna michezo ilivyo na nafasi kubwa kiuchumi,” ameongeza.

Aidha, ameeleza kuwa michezo ni sekta inayopendwa na inayotupatia nafasi kubwa ya kushiriki kimataifa na kupeperusha bendera ya taifa kwa fahari.

Related Articles

Back to top button