Mguu sawa michuano ya CAF

HATIMAYE imewadia tena wiki ya mechi za michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kwa ngazi za klabu, ambapo timu nne za Tanzania Bara na Visiwani leo zitakuwa dimbani kutafuta tiketi ya kupenya raundi inayofuata.
Mechi za leo ni mechi za marudiano baada ya mechi za awali zilizopigwa wikiendi iliyopita kwenye viwanja mbalimbali.
YANGA
Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara walianza vyema kwa kuitungua Zalan FC ya Sudan Kusini kwa mabao 4-0 katika mechi ambayo Yanga ilikuwa ugenini licha ya kupigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Ieleweke kuwa timu za Sudan Kusini zinazoumana na timu za Tanzania kwenye hatua hii ya awali, zinatumia viwanja vya Dar es Salaam kutokana na viwanja vya nchini kwao kutokidhi ubora unaohitajika na Caf katika michuano hiyo.
Kwa kauli rahisi unaweza kusema Yanga imetangulia hatua ya raundi ya kwanza mapema kutokana na matokeo yao hayo ya ‘ugenini’ na kilichobaki ni kukamilisha ratiba ikiwa nyumbani.
Udhaifu wa Zalan ulionekana dhahiri kuanzia hali yao kiuchumi, uliipa faida hiyo Yanga na sasa inatembea kifua mbele ikiwa imebakisa kazi ndogo kwenda hatua inayofuata.
Yanga haihitaji kujitutumua zaidi ya kuweka mambo yake kimkakati na kuimaliza mechi hiyo kwa wepesi ikitunza nguvu zake kwa ajili ya hatua inayofuata na michuano mingine inayowakabili.
Kulingana na mwanzo ilionao Yanga msimu huu, inaonesha inataka kitu na haipaswi kurudi nyuma na kwa namna ilivyotengeneza hesabu zake tangu mechi ya kwanza ni wazi mchezo umekwisha.
Kinachosubiriwa ni kukamilika kwa dakika 90 za mechi ya pili majira ya saa 1.00 jioni kisha hesabu ifungwe kikamilifu.
KMKM
Baada ya kuitazama Yanga, baadaye saa 3.00 usiku timu nyingine kutoka Zanzibar, KMKM itakuwa kibaruani dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Taifa wa Tripoli, mjini Tripoli.
KMKM watakuwa na kibarua kizito cha kupindua matokeo ya kubugizwa mabao 2-0 na mabingwa hao mara 12 wa Ligi Kuu ya Libya baada ya kukubali kichapo hicho ikiwa nyumbani Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Timu hiyo inayonolewa na Hemed Suleiman ‘Morocco’, ilionesha soka la kuvutia kama kawaida yake katika mchezo huo wa kwanza isipokuwa ilizidiwa ujanja kidogo na Walibya hao ambao walitangulia kwa bao la mkwaju wa penalti dakika ya 41 kabla ya kufunga la pili dakika ya 65.
Kulingana na uhalisia wa matokeo ya soka na hali ya upambanaji, inaonesha KMKM bado ina nafasi ya kujitetea na kufanya maajabu ikiwa ugenini kama wapinzani wao walivyofanya wakiwa Zanzibar.
KMKM si timu ngeni kwenye michuano hii, inafahamu changamoto, ujanja na mbinu kadhaa kuhusiana na mashindano hayo hivyo bado hawajachelewa, wana nafasi ya kuchanga upya karata zao na kurejesha furaha ya Wazanzibari.
GEITA GOLD
Geita ilikubali kipondo cha bao 1-0 ikiwa ugenini nchini Sudan dhidi ya Hila Alsahil na sasa watakuwa nyumbani kujiuliza ilikuwaje wakaruhusu kufungwa dakika ya 16 ya kwenye mechi hiyo ya awali.
Hii ni mara ya kwanza Geita kushiriki michuano ya Afrika kupitia Kombe la Shirikisho, lakini haikuonesha unyonge ikiwa ugenini na kupoteza kwa idadi ndogo kabisa ya mabao.
Ingawa Geita haijaonesha makali yake ya msimu uliopita ikikosa ushindi kwenye mechi tatu zilizopita za ligi, lakini haijapoteana kama inavyofikiriwa na ina uwezo wa kupindua matokeo katika mechi yao ya leo.
Kukosekana kwa mshambuliaji wao, George Mpole kwenye mechi ya awali pia inaonekana kama ni miongoni mwa sababu za kupoteza mchezo huo wa kwanza. Ugeni wa michuano pia inaonekana ni sababu nyingine.
Lakini bado ina kocha mzoefu wa mikikimikiki ya michuano mbalimbali Afrika na Tanzania, Fred Minziro. Yeye mwenyewe hajakata tamaa, anaamini nafasi ipo na kwa uzoefu alionao sio ajabu kama tutaiona Geita kwenye hatua inayofuata ya Kombe la Shirikisho Afrika.
KIPANGA
FC Timu nyingine kutoka Zanzibar inayowakilisha kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Timu hii kongwe ambayo ilipotea kwenye miaka ya hivi karibuni, imerejea kwa kishindo na imefanikiwa kutoa sare ya 1-1 kwenye mechi ya awali dhidi ya wapinzani wao wa Sudan Kusini, Al-Hilal Wau.
Kwenye mechi hiyo ambayo Kipanga ilikuwa ugenini kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam ilionesha uhai na kutoa ujumbe kwamba wana jambo kwenye michuano hii.
Mbali na uwezo waliokuwa nao lakini pia walionesha namna ya kutumia faida ya kucheza nyumbani mechi zote mbili kwa kutobweteka na kuwabana mbavu wapinzani wao wakisubiri kuwamaliza leo baadaye kwenye mechi itakayopigwa Uwanja wa Amaan.
Ingawa mechi yao bado ngumu kwa uhalisia wa matokeo, wanapaswa kucheza kwa nidhamu na kiwango cha hali ya juu kuhakikisha wanayalinda matokeo ya awali na kusonga mbele au kutafuta ushindi wa mapema na kutunza nguvu ya hatua inayofuata lakini bado kazi haijaisha.
SIMBA

Wekundu wa Msimbazi watakamilisha ratiba ya mechi hizo kwa timu za Tanzania kesho Jumapili kwa kuumana na Nyassa Big Bullets ya Malawi kwenye dimba la Mkapa.
Simba itaingia uwanjani majira ya saa 10 jioni ikiwa na faida ya ushindi wa mabao 2-0 ilioupata ilipokuwa ugenini wikiendi iliyopita katika mchezo ambao Simba ilicheza kwa nidhamu na ujanja wa hali ya juu ugenini.
Mara kadhaa ilikuwa ikipooza mpira na kuifanya Nyassa itulie wakati dakika zikiyoyoma na mwishowe ikafanikiwa kuwalaghai wapinzani na kuondoka na ushindi wa maana ugenini.
Hata hivyo, kwa ubora wa Nyassa bado Simba ina kazi ya kufanya katika mechi hiyo ikihitaji kuhakikisha wapinzani wao hawapati ushindi au kutibua matokeo kama walivyofanya wao walipokuwa ugenini.
Kocha mpya wa timu hiyo, Juma Mgunda ndiye aliyeiongoza Simba ugenini na sasa amebakiza dakika 90 kuweka rekodi ya kuivusha Simba kutoka hatua ya awali na kwenda raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwania kutinga hatua ya makundi kama ilivyozoeleka kwa timu hiyo katika miaka ya hivi karibuni.
Kwa ujumla matokeo ya timu zote yanaweza kuipa nafasi timu za Tanzania kusonga mbele lakini watahitaji umakini na kujitoa kwa kiwango cha juu mno ili kuendelea kuziweka klabu za Tanzania kwenye ramani ya michuano ya klabu Afrika.