Habari Mpya

Coastal Union yazitishia nyau Simba na Yanga

DAR ES SALAAM: Klabu ya ligi kuu ya Coastal Union imeziambia Yanga na Simba zijipange vilivyo kwa kuwa wanakuja kivingine kutaka kuvunja ufalme wa klabu hizo mbili kwa msimu wa 2024/25 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mwenyekiti wa Coastal Union, Steven Mguto ameiambia Spotileo, kuwa maandalizi ya yalianza mapema kwa kuimarisha kikosi kilichowafikisha nafasi ya nne, wanaimarisha zaidi kuwa bora kwa ajili ya kuingia kwenye vita vya kusaka nafasi mbili za juu ikiwemo Ubingwa.

Timu hiyo ambayo kwa sasa inashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika iliweka historia mwaka 1988 kwa kutwaa ubingwa ikiwa na wachezaji nyota kama, Mohammed Mwameja, Juma Mgunda, Ally Jangalu na Mohammed Kampira.

“Nia yetu msimu uliopita ilikuwa kutwaa ubingwa tukamaliza nafasi ya nne, kikosi kilichotufikisha hapa kimefanya kazi yake, lakini tunataka kutoka hapa na tupae juu zaidi ikiwezakana kufuta huu utawala wa hizi klabu za Yanga na Simba,” amesema Mguto.

Amesema wanafanya maboresho ya kikosi kwa kusajili wachezaji wanaokuja kusaidia timu kwenye mashindano waliyopo mbele yao, ikiwemo Kagame cup inayoanza leo, Ngao ya Hisani, Ligi Kuu Bara, Muungano na michuano ya kimataifa.

“Tuna mashindano takriban sita mbele yetu na tunataka kufanya vizuri ikiwemo kuingia kwenye vita vya ubingwa, kufikia huku lazima tuwe na kikosi imara kinamuwezesha mwalimu kutoa mtu na kuweka mtu bila hivyo hatuwezi kufanikiwa,” anasema Mwenyekiti huyo wa Coastal Union.

Ameeleza kuwa kutwaa ubingwa kwao haitamshangaza mtu kwa sababu wanarudia kwa kuwa waliwahi kutwaa taji hilo miaka ya nyuma na wanaimani kubwa ya usajili wanaoendelea kufanya utawasumbua wapinzani wao.

Coastal Union imeanza maandalizi ya msimu 2024/25 ikiwa ni miongoni mwa timu inayoshiriki mashindano ya kombe la Kagame limeanza kutimua leo, wanashuka dimba la KMC dhidi ya Dekadaha FC, saa 10:00 Alasiri.

Related Articles

Back to top button