Mfanyakazi mhamiaji afariki Kombe la Dunia
						MFANYAKAZI mhamiaji amefariki dunia wakati akifanya kazi katika eneo lililotumika kwa ajili ya mazoezi wakati wa hatua ya makundi katika michuano ya Kombe la Dunia 2022 inayoendelea Qatar.
Ripoti zimesema raia huyo wa Philippines anayesemekana kuwa na umri wa miaka 40 alihusika katika ajali ya mashine ya kunyanyua vitu vizito wakati akifanya ukarabati kwenye Hoteli ya ufukweni ya Sealine iliyokuwa ikitumiwa na timu ya Saudi Arabia.
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu(FIFA) limethibitisha tukio hilo lakini halijatoa taarifa yoyote zaidi hadi maelezo ya kina yatakapotolewa.
“FIFA imesikitishwa sana na msiba huu na mawazo na huruma yetu ziko kwa familia ya mfanyakazi,” imesema FIFA.
Mwezi uliopita Mkuu wa Kombe la Dunia Qatar 2022 Hassan Al-Thawadi amesema kumekuwa na vifo vya wafanyakazi wahamiaji kati ya 400 na 500 kwenye miradi inayohusiana na michuano hiyo.
Michuano ya Kombe la Dunia ipo katika hatua ya robo fainali ambapo Desemba 9 Croatia itakipiga na Brazil kabla ya Uholanzi kukiwasha dhidi ya Argentina.
				
					



