Messi, Son, Muller na Suarez wajitwisha MLS

NEW YORK: LIGI ya Soka ya Marekani (MLS) imesema kuwa msimu wake wa 30 umeonesha ongezeko kubwa la watazamaji na mahudhurio viwanjani, pamoja na kuongezeka kwa ushiriki na wafuasi wa kidijitali uliochangiwa na wachezaji kutoka ligi za Ulaya walioipa umaarufu zaidi.
Ligi hiyo ya Amerika Kaskazini imeshuhudia ongezeko la asilimia 29 la watazamaji wa matangazo ya moja kwa moja kwa wiki ikilinganishwa na msimu uliopita, huku idadi ya mashabiki waliohudhuria viwanjani ikifikia kiwango cha pili cha juu zaidi katika historia ya ligi hiyo.

Kwa mujibu wa MLS, mechi zake zilivutia wastani wa watazamaji milioni 3.7 kila wiki kupitia majukwaa ya televisheni na mitandao ya mtandaoni, ikiwemo Apple TV (MLS Season Pass), FOX Sports, TSN, RDS, Comcast, DirecTV, Amazon Prime Video, TikTok, EA FC Mobile na mashirika ya kimataifa.
Mahitaji ya tiketi kwenye viwanja pia yamesalia juu, ambapo jumla ya mashabiki milioni 11.2 wamehudhuria mechi za msimu wa 2025 wastani wa mashabiki 21,988 kwa kila mchezo huku klabu 19 vikivutia zaidi ya mashabiki 20,000 kwa kila mechi. Tangu 2022, mahudhurio ya jumla yameongezeka kwa asilimia 12.
Kwa upande wa majukwaa ya kidijitali, MLS imesema akaunti zake na za klabu zimeshuhudia rekodi ya ‘impressions’ bilioni 13.7 mwaka huu, ongezeko la asilimia 17 kutoka mwaka jana, huku wafuasi kwenye mitandao ya kijamii wakiongezeka kwa asilimia 10 na kufikia zaidi ya milioni 109.

Lionel Messi wa Inter Miami ameongoza mauzo ya jezi mwaka wa tatu mfululizo, akifuatiwa na Son Heung-Min wa LAFC aliyejiunga Agosti mwaka huu. Wengine waliokamilisha orodha ya tano bora ni Hirving “Chucky” Lozano (San Diego FC), Luis Suárez (Inter Miami) na Miguel Almirón (Atlanta United).
MLS imesema usajili wa Son umepelekea ongezeko la asilimia 16 la mashabiki kwenye mechi za ugenini za LAFC, huku ndani ya saa 72 baada ya kujiunga, Son akiwa mwanamichezo aliyenunuliwa bidhaa zaidi kwenye mtandao wa Fanatics.
Aidha, ligi iliongeza kuwa uwepo wa Son wa Korea Kusini na Thomas Müller wa Ujerumani ulisaidia kuongeza ‘impressions’ kwa asilimia 182 na ‘engagements’ kwa asilimia 193 katika kurasa za MLS, LAFC na Vancouver Whitecaps.




