Kwingineko

Messi kuiaga Argentina mbele ya Benin

BUENOS AIRES: MCHEZAJI Lionel Messi anatarajiwa kuaga rasmi soka la kimataifa akiwa na Argentina kesho, kupitia mchezo wa kirafiki dhidi ya Benin utakaopigwa kwenye Uwanja wa Monumental, Buenos Aires.

Messi mwenye umri wa miaka 39 anatarajiwa kucheza mechi yake ya mwisho akiwa amevaa jezi ya Argentina, huku mashabiki wapatao 85,000 wakitarajiwa kushuhudia tukio hilo la kihistoria.

Katika kipindi chake cha zaidi ya miaka 20 akiwa na timu ya taifa, Messi ameiongoza Argentina kutwaa Kombe la Dunia 2022, mataji mawili ya Copa America pamoja na Finalissima.

Messi anaondoka akiwa ndiye mchezaji mwenye rekodi ya mechi nyingi zaidi Argentina, akiwa amecheza mechi 207 na kufunga mabao 125, huku pia akiwa na rekodi ya pasi za mabao 68.

Mchezo huo pia utakuwa mwanzo wa kizazi kipya cha Argentina, huku wachezaji kama Cristian Romero, Alexis Mac Allister, Enzo Fernandez, Julian Alvarez na Lautaro Martinez wakitarajiwa kubeba majukumu makubwa baada ya Messi.

Kocha Lionel Scaloni amesema kizazi kipya kitaendelea kujenga Argentina bila Messi, ingawa amekiri kuwa si rahisi kuziba pengo la mchezaji huyo ambaye ametajwa na wengi kuwa miongoni mwa wachezaji bora zaidi katika historia ya soka.

Messi pia ataaga akiwa na baadhi ya wachezaji aliocheza nao kwenye safari ya kutwaa Kombe la Dunia 2022, akiwemo Angel Di Maria, ambaye tayari alistaafu soka la kimataifa mwaka 2024.

Kwa sasa Messi bado ana mkataba na Inter Miami hadi 2028, lakini amewahi kutoa ishara kwamba anaweza kumaliza kabisa safari yake ya soka mapema kuliko ilivyotarajiwa.

Kikubwa kinachosubiriwa baada ya kuaga kwake ni nani atakabidhiwa jezi namba 10 ya Argentina, ambayo kwa zaidi ya muongo mmoja imekuwa ikihusishwa na jina la Messi.

Related Articles

Back to top button