BurudaniFilamu

MEMORIES

KILA mwaka maelfu ya filamu zinatolewa duniani kote na kila filamu ina aina yake ya usimuliaji; zipo filamu za kuchekesha, za mapigano, za kutisha, zenye taharuki, za kusisimua, za mapenzi, za upelelezi, za uchawi, njozi na aina nyingine nyingi.

Kama wewe ni mpenzi wa kutazama filamu za kihalifu au za kipelelezi zenye taharuki, hasa kutoka tasnia ya filamu ya India (Bollywood), basi filamu ya ‘Memories’ iliyotengenezwa kwa lugha ya Kimalayalam, nchini India na kutolewa mwaka 2013 inakufaa sana.

Kisa cha filamu hii kinamwonesha jamaa fulani, Sam Alex (nafasi iliyochezwa na Prithviraj Sukumaran), ofisa wa polisi anayeishi kwa kutegemea ulevi wa pombe ili kupunguza maumivu ya kupoteza familia yake.

Kabla, Sam Alex alikuwa kijana mtanashati kwelikweli na mwenye familia bora, akiishi maisha ya furaha na familia yake. Mke wake, Teena na binti wao mdogo waliuawa na adui mbele ya macho yake, na matokeo yake, Sam anaamua kujitumbukiza kwenye ulevi wa kupindukia.

Kwa kuwa anazo fedha, anaamua kukaa mbali na kazi kwa muda mrefu huku akitumia muda mwingi kulewa.

Katika kipindi hicho anachojitenga na kazi yake, yanatokea mambo ya kushangaza na yanawachanganya sana polisi, vijana kadhaa waliooa wanatoweka mmoja baada ya mwingine na kuuawa.

Mwalimu na baba wa Sam, Aravindhaksha Menon (nafasi inayochezwa na Vijayaraghavan) anajaribu kumwomba Sam kuchukua jukumu la kuchunguza vifo hivyo, kwa kuwa polisi waliopewa jukumu la kuchunguza wanashindwa kufanikiwa.

Menon anafanya hivyo akitarajia kuwa hiyo inaweza kuyafanya maisha ya Sam kurudi katika hali ya kawaida.

Sam anakataa kuchukua jukumu hilo hadi pale mama yake (Vanitha Krishnachandran) anapoingilia kati kumshawishi ili akubali jukumu hilo, na Sam anakubali lakini anatoa sharti kwamba asizuiwe kunywa pombe.

Kisha anajitosa katika upelelezi na kuanza kukusanya pamoja ushahidi wa visa vya ajabu vya muuaji huyo huku pombe anayokunywa ikifungua mlango wake wa sita wa fahamu.

Katika harakati hizo anayachunguza mafaili ya kesi na kutazama nyaraka za matokeo ya uchunguzi wa maiti (postmortem) na baadaye kutaka ushauri kwa madaktari waliofanyia uchunguzi maiti hizo.

Ni hapo ambapo Sam anaona mwanga wa mafanikio katika kesi hiyo. Katika muda huo watu wengine wawili wanatekwa katika mfululizo wa visa hivyo na yote haya yanasababisha hitimisho baya kwa mwuaji (S.Sreekumar).

Sam anagundua kuwa mwuaji ni mtu anayetembea kwa kuchechemea na ni mtu ambaye ama anawachukia au kuwapenda sana wanawake. Na kila yanapotokea mauaji basi mwuaji huyo huacha alama fulani zilizoandikwa kwa kisu kikali kwenye kifua cha aliyemuua.

Hii inamfanya Sam kufikiria mbali zaidi kuhusu aina ya mwuaji alivyo na nani anayefuatia katika mauaji hayo. Anapochunguza kwa makini maandishi yaliyoandikwa katika miili ya waathirika, anagundua kwamba ni maneno ya Kiaramu, lugha ambayo Yesu aliitumia kwa mawasiliano.

Anagundua kuwa ni maneno yanayoelezea mithali za Kibiblia, kwa hiyo inamsaidia zaidi Sam katika kupata hitimisho kwamba mwuaji huyo ni mtu aliyechanganyikiwa na kwamba anadhani kuwa waathirika hao wametoa maisha yao kwa ajili ya dhambi zilizofanywa na wake zao.

Sam hachelewi kugundua kwamba wanawake wote ambao waume wao wameuawa wanafahamiana na wote waliwahi kuwa na uhusiano na mwanamume mmoja waliyesoma naye miaka kadhaa huko nyuma.

Wakati akiendelea na upelelezi wake, anagundua kuwa kuna mlengwa mmoja wa mwisho katika mlolongo huo na mwuaji akimmaliza huyo basi atatoweka na asionekane tena.

Anagundua kwamba mlengwa anayefuatia katika mtiririko wa mauaji hayo ni mdogo wake aitwaye Sanju, na kwamba mke wa Sanju ndiye mtu wa mwisho katika uhusiano miongoni mwa wale wanawake.

Hivyo anaamua kwenda huko kwa pambano moja la mwisho… Je, nini hatma ya yote haya? Sam atafanikiwa kumnasa mwuaji au naye ataingia kwenye orodha ya waathirika? Katika filamu hii ya kusisimua, Sam anajitahidi sana kuonekana muungwana licha ya ulevi wake.

Baadhi ya nadharia anazotekeleza katika upelelezi wake zinatokea bila kutarajiwa. Hata hivyo, kuna pengo katika usukaji wa visa vya hadithi (plot), ambalo linamfanya mtazamaji ajiulize endapo mwongozaji wa filamu aliteleza, au labda mhariri wa filamu hii aliamua (kwa makusudi) kupunguza vitu muhimu ili filamu iende spidi. P

amoja na filamu kusisimua lakini script ina mapengo mengi na haitoi majibu yenye kushawishi kwa maswali yanayoibuka pindi uitazamapo filamu hii. Vinginevyo, si vibaya kama ukiitafuta.

Related Articles

Back to top button