Muziki

Megan Thee Stallion: mitandao ya kijamii imerahisisha umaarufu

NEW YORK: RAPA wa kimataifa, Megan Thee Stallion, amesema kuwa ukuaji wa mitandao ya kijamii umebadilisha tasnia ya muziki kwa kiasi kikubwa, akieleza kuwa kwa sasa mtu anaweza kupata umaarufu mkubwa hata bila kuwa na kazi bora za muziki.

Megan amesema tofauti na zamani ambapo wasanii walipaswa kujitahidi zaidi kupitia ubora wa kazi zao ili kutambulika, siku hizi mitandao ya kijamii imekuwa njia rahisi ya kuwafanya watu wengi kujulikana kwa muda mfupi.

“Kiukweli, kwa sasa ni rahisi kuwa maarufu. Unaweza kuwa maarufu sana mtandaoni, hasa kwenye majukwaa kama Instagram, hata kama una wimbo ambao si mzuri,” amesema Megan.

Msanii huyo ameeleza kuwa mitandao ya kijamii imefungua fursa nyingi kwa wasanii na wabunifu wa maudhui, lakini pia imeleta changamoto ya kutenganisha umaarufu wa muda mfupi na vipaji vya kweli.

Amesema kuwa katika mazingira ya sasa, baadhi ya watu hujikita zaidi katika kutafuta umaarufu kuliko kuwekeza katika kuboresha kazi zao, jambo ambalo linaifanya tasnia kuwa na ushindani wa aina tofauti na ule wa zamani.

“Mitandao imefanya iwe rahisi sana kuwa maarufu, iwe kwa njia nzuri au mbaya. Nadhani unaweza kutofautisha kati ya watu wanaopenda kweli wanachokifanya na wale wanaotaka tu kuwa maarufu,” amesema.

Megan ameongeza kuwa yeye anajiona kuwa miongoni mwa wasanii wanaofanya muziki kwa sababu ya mapenzi ya kazi hiyo, badala ya kutafuta umaarufu pekee.

Kauli hiyo imeibua maneno miongoni mwa wadau wa muziki duniani, huku wengi wakikubaliana kuwa mitandao ya kijamii imekuwa na mchango mkubwa katika kuibua vipaji vipya, lakini pia imefanya umaarufu kupatikana kwa urahisi kuliko ilivyokuwa hapo awali.

Kwa sasa, Megan Thee Stallion anaendelea kuwa mmoja wa wasanii wa kike wenye ushawishi mkubwa katika muziki wa Hip Hop duniani, akitambulika kwa nyimbo zake zilizofanikiwa kufanya vizuri katika chati mbalimbali za muziki kimataifa.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button