Afrika Mashariki

Mchezaji mpya wa Gor Mahia atoa neno kwa mashabiki

NAIROBI: USAJILI mpya wa timu ya soka ya Gor Mahia, Mike Kibwage amesema shinikizo kutoka kwa mashabiki wanaohitaji ushinidi utamfanya kuwa mchezaji bora wa timu hiyo mpya.

Kibwage anasema mazingira ya ushindani kama yale ya mabingwa hao mara 21 wa Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) yatamlazimisha kuinua kiwango chake.

“Matarajio yangu ni kudumisha nafasi yangu katika timu ya taifa na kuwa katika klabu kama K’Ogalo kutanisaidia kufanikisha hilo. Katika ngazi ya kitaifa, kuna mashabiki wengi wanaotaka kuona timu ya taifa ikifanikiwa. Ni sawa na hapa Gor na shinikizo kutoka kwa mashabiki litanisaidia tu kuwa bora,” beki huyo wa kati alisema.

Kibwage ametia wino mkataba wake na timu hiyo mpya, baada ya kukamilisha miaka miwili ya kusalia na Tusker FC, ambayo alijiunga nayo 2023 kutoka Sofapaka.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 amewahi kuzichezea AFC Leopards na Kenya Commercial Bank (KCB).

Akitafakari kuhusu uamuzi wake wa kuwaacha watengenezaji bia, Kibwage aliamini kuwa ni hamu yake ya kujaribu changamoto mpya.

“Mwishowe, ilinibidi kuwa na ujasiri kuhusu hilo na kufanya uamuzi wa kuhama. Nimekuwa kwenye klabu ya juu kwa muda lakini sasa nilihisi ni wakati wa kujaribu changamoto kubwa zaidi, ikiwa si sawa na klabu niliyokuwa hapo awali,” alisema.

Kibwage anajiunga na Gor kutokana na matokeo mazuri katika Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) ambapo alikuwa sehemu ya timu ya Harambee Stars iliyoweka historia ya kufika robo katika mechi yao ya kwanza katika michuano hiyo.

Beki huyo wa kati ataungana na wachezaji wenzake wa Harambee Stars akiwemo Sylvester Owino, Alphonce Omija, Mohammed Siraj, Lewis Bandi, Austine Odhiambo na Felix Oluoch.

Gor wanaunda upya kikosi chao chini ya kocha mkuu mpya Charles Akonnor baada ya kumaliza msimu wa 2024/25 bila taji.

Related Articles

Back to top button