McClaren abwaga manyaga Jamaica

KINGSTON: KOCHA wa zamani wa timu ya Taifa ya England, Steve McClaren, amejiuzulu kama kocha wa timu ya Taifa ya Jamaica baada ya “Reggae Boyz” kulazimishwa sare ya 0-0 dhidi ya Curaçao na kushindwa kufuzu moja kwa moja Kombe la Dunia la 2026.
Matokeo hayo yalimaanisha Curaçao kuongoza Kundi B kwa CONCACAF na kwenda mashindano hayo kwa mara ya kwanza katika historia yake, taifa hilo dogo zaidi kwa idadi ya watu limeweka rekodi ya kuwa taifa dogo zaidi kufuzu Kombe la Dunia.
Itajiunga na mataifa mengine ya CONCACAF yaPanama na Haiti ambayo pia yamekamilisha kufuzu. Jamaica ilimaliza nafasi ya pili katika Kundi B lakini bado inaweza kuendelea kufuzu Kombe la Dunia kupitia mlango wa Playoff.

Michezo ya Jumanne ilihitimisha timu sita ambazo zitashiriki michezo ya mtoano ya kimataifa huko Mexico Machi mwaka ujao. Timu mbili zitafuzu kupitia michezo hiyo, ikiwemo Iraq kutoka Asia, Congo kutoka Afrika, Jamaica na Suriname kutoka CONCACAF, Bolivia kutoka Amerika Kusini na New Caledonia kutoka Oceania.
McClaren amejiuzulu muda mchache tu baada ya mchezo huo uliopigwa jijini Kingston, akisema uamuzi wake ni kwa maslahi mapana ya timu.
“Kati ya miezi 18 iliyopita nimefanya kila nilichoweza kwenye kazi hii Kuwa kiongozi wa timu hii imekuwa heshima kubwa zaidi katika taaluma yangu.” Amesema
McClaren alichukua nafasi hiyo baada ya kuondoka Manchester United katika majira ya joto ya Ulaya mwaka 2024, ambapo alihudumu kama kocha msaidizi wa Erik ten Hag.




