Kwingineko

Mbappe kusubiri 16 bora CWC

PHILADELPHIA, Kocha wa Real Madrid Xabi Alonso amethibitisha kuwa mshambuliaji wa klabu hiyo Kylian Mbappe ataukosa mchezo wa mwisho wa Real Madrid katika hatua ya makundi Kombe la Dunia la Klabu dhidi ya RB Salzburg huku akiendelea kupata nafuu kutokana na ugonjwa akisema anapaswa kuwa tayari kwa hatua ya mtoano kama watavuka.

Mshambuliaji huyo wa Ufaransa tayari alirejea mazoezini mapema Jumatano baada ya kupona ugonjwa wa gastroenteritis aliougua wiki iliyopita, lakini Alonso anasema uamuzi wa kutomjumuisha katika mechi hiyo ya Ijumaa alfajiri umefanywa kwa maslahi ya mchezaji ili aweze kupona kabisa.

“Ilikuwa siku yake ya kwanza mazoezini, siku yake ya kwanza kukimbia kidogo, na alifanya vizuri, Lakini bado hajapona kabisa bado hana utimamu wa kucheza na Salzburg”

“Tulizungumza baada ya mazoezi na alisema anapendelea kupumzika zaidi na kupona ipasavyo na kwa wakati. Na ikiwa tutafika hatua ya 16 bora atakuwepo, lakini bado yupo katika harakati za kupona na hayuko fiti kwa mchezo huu.” – Alonso amewaambia wanahabari katika uwanja wa Lincoln Financial Field jijini Philadelphia

Mbappe ambaye alipata matibabu katika hospitali moja mjini Miami wiki iliyopita, tayari amekosa sare ya 1-1 ya Real Madrid na Al-Hilal na ushindi wao wa 3-1 dhidi ya Pachuca, ushindi walioupata licha ya kucheza mechi hiyo wakiwa na wachezaji 10 uwanjani.

Wahispania hao wanaongoza Kundi H wakiwa na pointi nne, mbele ya Salzburg kwa tofauti ya mabao, huku Al-Hilal wakiwa na pointi mbili na Pachuca bado hawajapata pointi moja.

Related Articles

Back to top button