Mbappe atemwa tena timu ya taifa

NAHODHA wa timu ya taifa ya Ufaransa na staa wa Mabingwa wa soka la Ulaya Real Madrid Kylian Mbappe, hajajumuishwa katika kikosi kitakachocheza mechi zinazokuja za UEFA Nations League dhidi ya Israel na Italia katika kikosi kilichotangazwa muda mfupi uliopita.
Hii ni mara ya pili kwa Mbappe kutokuwepo kwenye kikosi cha kocha Didier Deschamps baada ya nyota huyo kutokuwepo kwenye michezo ya mwezi Oktoba dhidi ya Israel na Ubelgiji.
Nyota huyo mwenye miaka 25 alipumzishwa katika mechi hizo ili kumpa nafasi apone jeraha la paja alilopata akiitumikia klabu yake ya Real Madrid hata hivyo suala hilo lilizua utata baada ya Mbappe kuonekana uwanjani akiitumikia Real Madrid siku chache kabla ya mechi za timu ya taifa.
Baada ya kukosekana kwenye ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Israel na 2-1 dhidi ya Ubelgiji nyota huyo alienda mapumzikoni jijini Stockholm nchini Sweeden. Tangu kipindi hicho nyota huyo wa zamani wa PSG amecheza mechi kadhaa na klabu yake akifunga goli moja pekee.