MasumbwiMichezo Mingine

Mbabe wa Dulla Mbabe sasa amtaka Kiduku

BAADA ya Bondia wa Jamhuri wa Kidemokrasia ya Congo (DRC), Tshimanga Katompa kumpa kichapo, Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’, amesema sasa anamtaka Twaha Kiduku amuoneshe kazi.

Kauli hiyo imemfikia Kiduku na kusema yupo tayari kupambana naye ili amnyooshe.
“Salam zimenifikia mapromota leteni kazi nimshooshe, hili gari la shamba linapita kokote sio kama hao wanaochagua nani wa kucheza naye,” alisema kupitia ujumbe aliouweka katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram.

Alisema iwapo pambano hilo litaandaliwa atamlipia kisasi Dulla Mbabe kwa kuhakikisha anashinda.

Katompa alisema bondia anayemuhitaji kwa sasa ni Kiduku na kwamba anamfahamu vizuri na yuko tayari kumgaragaza kama ilivyokuwa kwa Dulla Mbabe.

Alisema atakapofanikiwa kupata nafasi ya kupambana na Kiduku hatakuja na staili aliyommaliza Dulla Mbabe, kwani ana mbinu nyingi kwa hiyo atarudi kivingine.
Kiduku alicheza pambano lake la mwisho dhidi ya Dulla Mbabe na kushinda gari lililokuwa likiwaniwa aina ya Toyota Crown Athlete.

Katika hatua nyingine, Dulla Mbabe amesema bado yupo sana kwenye ngumi, bali atapumzika miezi miwili kisha atarejea usiku wa mabingwa Desemba.

Bondia huyo baada ya kupoteza pambano lake wadau walimtaka aache ngumi.
Kufuatia kushindwa kwa kipigo cha aibu, Dulla Mbabe aliwaomba Watanzania radhi na kuwataka wamtie moyo badala ya kuendelea kutoa lugha za matusi na kejeli dhidi yake kwenye mitandao ya kijamii.

“Samahani kama kuna mtu amekasirika, mimi ni mpambanaji, naomba Watanzania tupeane moyo, tuache matusi na kashfa kwenye mitandao ya kijamii,”alisema.

Related Articles

Back to top button