Mawazo ya salah sasa ni AFCON

CAIRO: KIUNGO mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah, atapumzika presha ya Anfield wiki ijayo atakapojiunga na timuu ya Taifa ya Misri kuelekea Morocco kwa ajili ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), licha ya sintofahamu iliyozuka baada ya kutofautiana na kocha wake Arne Slot.
Kocha wa Misri Hossam Hassan alimhakikishia nahodha huyo nafasi kwenye kikosi baada ya kutaja kikosi cha wachezaji 28 Alhamisi jioni, kwa ajili ya michuano inayoanza Desemba 21. Hivyo, Salah, mwenye miaka 33, atakosa angalau mechi mbili za Ligi Kuu England.
Tangu sare ya wikiendi iliyopita dhidi ya Leeds United, Salah amekuwa Habari kuu kwenye vyombo vya habari baada ya kudai kwamba amekuwa kichacheo cha lawama kwa matokeo duni ya Liverpool, na kudokeza kuwa uhusiano wake na Slot umeingia doa.
Salah hakucheza dhidi ya Leeds wala West Ham United, na pia hakujumuishwa kwenye ushindi wa 1-0 dhidi ya Inter Milan katikati ya wiki kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hata hivyo, atapatikana kwenye mchezo dhidi ya Brighton Jumamosi, baada ya FIFA kubainisha kwamba wachezaji wanapaswa kuripoti kambini kwa timu zao za taifa wiki moja tu kabla ya AFCON kuanza. Liverpool itacheza na Tottenham Hotspur na Wolverhampton Wanderers wakati Misri ikiendelea na hatua ya makundi.
Mshambuliaji wa Manchester City Omar Marmoush pia ameitwa, sambamba na winga wa Al-Ahly na aliyewahi kucheza Aston Villa, Mahmoud Trezeguet.
Misri mabingwa wa Afrika mara saba, wataanza kampeni yao kwa kuvaana na Zimbabwe Desemba 22, kisha Afrika Kusini Desemba 26, kabla ya kumaliza hatua ya makundi dhidi ya Angola Desemba 29.
Kikosi Kamili cha Misri – AFCON 2025
Makipa:
Mohamed El-Shenawy (Al-Ahly), Ahmed El-Shenawy (Pyramids), Mostafa Shobeir (Al-Ahly), Mohamed Sobhi (Zamalek)
Mabeki:
Mohamed Hany (Al-Ahly), Ahmed Eid (El-Masry), Rami Rabia (Al-Ain), Khaled Sobhi (El-Masry), Yasser Ibrahim (Al-Ahly), Mohamed Ismail (Zamalek), Hossam Abdelmaguid (Zamalek), Mohamed Hamdy (Pyramids), Ahmed Fatouh (Zamalek)
Viungo:
Marwan Ateya (Al-Ahly), Hamdy Fathy (Al-Wakrah), Mohanad Lasheen (Pyramids), Mahmoud Saber (Zed), Mohamed Shehata (Zamalek), Emam Ashour (Al-Ahly), Ahmed Zizo (Al-Ahly), Mahmoud Trezeguet (Al-Ahly), Ibrahim Adel (Al-Jazira), Mostafa Fathi (Pyramids), Omar Marmoush (Manchester City), Mohamed Salah (Liverpool)
Washambuliaji:
Mostafa Mohamed (Nantes), Salah Mohsen (El-Masry), Osama Faisal (National Bank of Egypt)



