Kwingineko

Mashabiki walia na bei za tiketi WC 2026

WASHINGTON: MASHABIKI wa soka duniani wameishambulia FIFA vikali wakilaani kile walichokiita usaliti mkubwa baada ya bei mpya za tiketi za Kombe la Dunia kuanza kuzunguka mitandaoni mapema Alhamisi.

Kwa utaratibu wa kawaida, FIFA hutenga asilimia 8 ya tiketi kwa mashirikisho ya kitaifa ili ziuzwe kwa mashabiki wa timu husika. Hata hivyo, orodha iliyochapishwa na Shirikisho la Soka la Ujerumani imeibua taharuki kubwa kutokana na viwango vya juu vya bei.

Tiketi za mechi za hatua ya makundi zinakadiriwa kugharimu kati ya dola 180 hadi 700, huku mechi ya fainali ikiuzwa kuanzia dola 4,185 hadi dola 8,680. Viwango hivyo viko mbali na ahadi ya FIFA ya tiketi za dola 60, pamoja na matarajio ya wenyeji wa Marekani ambao waliahidi nafasi za tiketi dola 21 wakati wa kuomba uenyeji miaka saba iliyopita.

Chama cha Mashabiki wa Soka Ulaya (FSE) kimezikosoa vikali bei hizo na kuzieleza kama za kikatili na zinazopuuza mchango wa mashabiki katika hadhi ya Kombe la Dunia.

Wakati huo huo, Shirikisho la Soka la England (FA) limewapa taarifa wanachama wa England Supporters Travel Club (ESTC) ikionesha kuwa shabiki atakayefuata timu hadi fainali angetumia zaidi ya dola 7,000 kwa tiketi pekee.

FIFA, kupitia taarifa za awali Septemba, ilisema tiketi za mtandaoni zitauzwa kuanzia dola 60 hadi 6,730, lakini ikasisitiza bei hizo zinaweza kubadilika kutokana na mfumo mpya wa ‘dynamic pricing’ unaotumika kwa mara ya kwanza kwenye mashindano ya Kombe la Dunia.

Katika bei za Ujerumani, kulionekana kategori tatu pekee, ikiwemo tiketi ya bei ya chini kabisa ya dola 180 kwa mechi ya ufunguzi ya Ujerumani dhidi ya Curaçao huko Houston. Kwa nusu fainali, tiketi za chini zilikuwa dola 920 na zile za juu hadi dola 1,125.

FSE imeitaka FIFA kusimamisha mara moja uuzaji wa tiketi kupitia mashirikisho ya kitaifa hadi pale suluhisho linaloheshimu hadhi, historia na upekee wa Kombe la Dunia litakapopatikana.

FIFA bado haijatoa taarifa yeyote au maoni juu ya suala hilo.

Related Articles

Back to top button