EPL

Man City yashusha mrithi wa De Bruyne

MANCHESTER: KLABU ya Manchester City imekamilisha usajili wa kiungo wa kati wa Netherlands Tijjani Reijnders kutoka AC Milan kwa dau la pauni milioni 46.3 huku akimwaga wino kuwatumikia washiriki hao wa kombe la Dunia la Klabu kwa miaka mitano.

Kuwasili kwa Reijnders mwenye miaka 26 kunafanya idadi ya wachezaji waliosajiliwa na Man City kuwa wanne ndani ya wiki moja, ambapo tayari wametangaza mikataba ya kiungo wa kati Rayan Cherki kutoka Lyon kwa pauni milioni 30.5 na kipa namba tatu wa Chelsea, Marcus Bettinelli huku beki wa kushoto Rayan Ait-Nouri akijiunga kutoka Wolves kwa uhamisho wa pauni milioni 31.3.

Reijnders anawasili City baada ya kufanya vizuri katika msimu tata kwa klabu yake ya zamani AC Milan, ambao walimaliza katika nafasi ya nane kwenye Serie A na kukosa nafasi ya kukiwasha kwenye Ligi ya Mabingwa barani ulaya msimu ujao. Uhamisho huo umekamilika kwa wakati ili wachezaji kusajiliwa kwa ajili ya hatua ya makundi ya Kombe la Dunia la Klabu linaloanza Jumapili.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba Reijnders amesema anafuraha kutua katika klabu hiyo yenye kocha bora, wachezaji wa kiwango cha juu na miundombinu bora zaidi ya soka barani ulaya huku akielezea tamanio lake la kurejesha mataji Etihad.

“Nina furaha sana kusajiliwa Manchester City. City ni moja ya timu kubwa duniani, ikiwa na kocha bora, wachezaji wa kiwango cha kimataifa na vifaa bora. Chini ya Pep Guardiola, City wameshinda mataji mengi na ninataka kusaidia kuendeleza hilo kwa mafanikio makubwa katika miaka ijayo. Pia ndoto imetimia kucheza Premier League.” Amesema

Katika msimu uliomalizika wa 2024/25 Reijnders amecheza michezo 54 ya mashindano yote akihusika na mabao 20. Mabao 15 akifunga kwa mguu wake na akitoa asisti 5. Bila shaka mashabiki wa man city wanatarajia ataimarisha safu ya kiungo ya Pep Guardiola baada ya kuondoka kwa Kevin De Bruyne.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button