Makipa wa kigeni ruksa K-League

SEOUL: Bodi inayosimamia Ligi kuu ya soka ya Korea Kusini maarufu kama K-League imeondoa marufuku ya miaka 26 kwa makipa wa kigeni kucheza katika ligi hiyo kongwe zaidi barani Asia kuanzia msimu mpya wa 2026.
Makipa wa taifa hilo pekee ndio waliruhusiwa kucheza katika Ligi hiyo tangu mwaka 1999 Sheria hiyo ikianzishwa kwa nia ya kulinda vipaji vya wazawa kwakuwa wakati huo kulikuwa na Klabu 10 ‘professional’ kwenye ligi hiyo.
Maamuzi hayo yalitangazwa baada ya mkutano mkuu wa bodi hiyo uliofanyika jijini Seoul wiki hii kuamua kwamba kwa sababu sasa kuna Klabu 26 zinavyoweza kucheza ‘professional’ kwenye ngazi mbili za juu za mashindano ya klabu nchini humo, kuna nafasi ya kutosha kwa makipa wa kimataifa.
“Kuongezeka kwa idadi ya Klabu kunamaanisha kuwa kuna fursa za kutosha kwa makipa wa ndani kucheza hata kama makipa wa kigeni wanaruhusiwa. Tumezingatia ukweli kwamba kutokana na usajili wa wachezaji wa kigeni kuwekewa vikwazo, kiwango cha nyongeza cha mishahara ya makipa wa ndani kimeongezeka kwa kiasi kikubwa.” – bodi ilisema katika taarifa yake.
Kulikuwa na wasiwasi kutokana na kuongezeka kwa ukubwa wa orodha za vikosi za kisasa ambazo zina makipa watatu au wanne kwamba kuna uhaba wa makipa bora nchini humo. Hatua hiyo itaiweka K-League sambamba na ligi nyingine kubwa za bara la Asia kama za Japan, Saudi Arabia na China.