Majaliwa: “Serikali imelenga ongezeko la Viwanja bora”

DAR ES SAALAM: WAZIRI Mkuu Jamhuri ya Muungano wa Kassim Majaliwa amesema lengo la Serikali kutoa tozo za nyasi bandia wanataka kuona viwanja vingi vya Tanzania vinakuwa na hadhi na ubora wa kimataifa.
Amesema hayo katika katika hafla ya utoaji tuzo zilizoandaliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), zilizofanyika katika Ukumbi wa The Super Dome, Masaki, Dar Es Salaam.
Majaliwa amesema kutokuwepo kwa tozo ya nyasi bandia itasaidia kujengwa kwa viwanja vingi hasa kuelekea katika maandalizi ya mashindano ya Mataifa ya Afrika ‘AFCON’, 2027, Tanzania ambao ni wenyeji sambamba na nchi za Kenya na Uganda.
“Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha sekta ya michezo inapewa kipaumbele kutokana na kuwa ya muhimu inaleta maendeleo ya taifa, suala la viwanja tayari kuna maboresha makubwa yanafanyia uwanja wa Benjamini Mkapa, Uhuru na New Amaan Complex, Visiwani Zanzibar,’” amesema.
Ameongeza kuwa wanajenga uwanja Mwanza, Arusha, Tanga, Mbeya na Dodoma kwa ajilia ya maandalizi ya AFCON, jambo la kujivunia Tanzania kupata fursa ya kuendesha mashindano makubwa kama hayo ambayo imetokana na juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuhakikisha nchi yetu inafika mbali kupitia michezo.
Amesema sekta ya Michezo inachangia kwa kiasi kikubwa kutoa ajira kwa vijana, kuchangia pato la taifa, lakini inapunguza gharama za matibabu kwa maradhi yasiyoambukiza.
Pia amesema kuwa sekta ya Michezo inalitangaza taifa la Tanzania duniani, inaleta burudani na hamasa pamoja na kujenga umoja wa kitaifa.
“Fedha inayotengwa kwa ajili ya shughuli za michezo hususan asilimia tano ya mfuko wa maendeleo ya michezo itumike kama ilivyokusudiwa ili kuendelea kuinua michezo nchini,”
“Tumpongeze na kumshukuru sana rais, Samia, kwa kuthamini michezo na utamaduni, nitoe maagizo kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo iandae programu mbalimbali za michezo ambazo zitakuza vipaji kwa Watanzania kuanzia ngazi ya elimu ya awali,” amesema.
Amesisitiza kuwa mamlaka ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia zihakikishe michezo inachezwa kikamilifu katika ngazi zote za shule ikiwemo ya Awali, Msingi, Sekondari pamoja na Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati, wahakikishe wanashiriki katika kuendeleza michezo ipasavyo.