Mabondia Kibangaze, Omar kukiwasha kimataifa

DAR ES SALAAM:BARAZA la Michezo la Taifa (BMT) limewatakia kila la heri mabondia Jemsi Kibangaze na Mohamed Omari wanaotarajiwa kuwakilisha nchi kimataifa.
Kibangaze anatarajiwa kupanda ulingoni Juni 14, mwaka huu ugenini nchini Uingereza dhidi ya bondia Mikie Tallon wa Uingereza katika pambano la raundi nane uzito wa kilo 52 litakalopigwa Greenbank sports academy, Liverpool.
Takwimu zinaonesha Kibanzange kwa miaka ya karibuni hilo litakuwa ni pambano lake la nne. Amecheza mapambano matatu na mabondia tofauti nchini humo hajashinda.
Mtandao wa boxrec unaonesha Mtanzania huyo ni bondia mzoefu aliyecheza jumla ya mapambano 34 ya ndani nan je na kati ya hayo, ameshinda 21, amepoteza 10 na kupata sare tatu.
Aidha, Omari atakuwa Ghana Juni 13, mwaka huu nchini Ghana dhidi ya bondia Ohara Dvies katika pambano la raundi 6 uzito wa kilo 66.
Omar ni bondia chipukizi na takwimu zinaonesha hilo litakuwa ni pambano la kwanza la kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa ya BMT: “Tunawatakila kila la heri Kibangaze na Omari, Watanzania tuwaunge mkono kwa dua na maombi,”
				
					



