Lulu afunguka kuhusu changamoto za utotoni

DAR ES SALAAM: MSANII nyota wa filamu nchini Tanzania, Elizabeth Michael ‘Lulu’, ameibua mjadala mtandaoni baada ya kufunguka kuhusu maisha yake, changamoto alizopitia na namna anavyojihusianisha na nyota yake ya Aries.
Kupitia ukurasa wake wa Snapchat, Lulu alieleza kuwa watu wa nyota ya Aries mara nyingi hupitia mapambano makubwa maishani, kutokana na hatima kubwa waliyonayo kiastrology.
“Niliwahi kusoma sehemu kwamba, katika zodiac zote 12, Aries ndiyo nyota yenye vita kubwa sana kuliko zote.
Kiastrology wanasema ni kwa sababu Aries wengi wana hatma kubwa,” ameandika Lulu.
“Vita inapokuwa kubwa, lazima hatma nayo iwe kubwa. Na Mungu akikuvusha salama ukazishinda, ushindi unakuwa mkubwa pia.
Sehemu ngumu ni kukubali majaribu, kusikiliza sauti ya Mungu, kujifunza katika hayo majaribu na kurekebisha makosa pia kujitahidi kuepuka baadhi ya vitu vilivyo ndani ya uwezo.”
Lulu pia ametumia nafasi hiyo kugusia malezi ya utotoni na jinsi yanavyoweza kuathiri ukuaji wa watu wa nyota hiyo, akisema wengi wao hupitia changamoto nyingi tangu wakiwa wadogo.
“Mungu atusaidie, maana Aries kuanzia kwenye malezi yetu wengi inakuwa misukosuko… yani naona shege kuanzia utotoni, na ndiyo maana ukikuta Aries ambaye hajaheal, ni mtu hatari sana,” ameandika.
Ujumbe huo wa Lulu umevuta hisia za mashabiki wake mitandaoni, wengi wakimsifia kwa ujasiri wa kuzungumza waziwazi kuhusu safari yake ya maisha na kuhusisha imani, nyota na uzoefu binafsi.




