Ludacris kusherehesha tuzo za muziki 2026

LOS ANGELES: RAPA, muigizaji na mfanyabiashara maarufu nchini Marekani Christopher Brian ametangazwa rasmi kuwa mtangazaji mkuu wa tuzo za muziki za iHeartRadio 2026, tukio linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa muziki duniani.
Tukio hilo linatarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Dolby Theatre uliopo jijini Los Angeles, nchini Marekani.
Katika tuzo hizo mwanamuziki na muigizaji Miley Cyrus anatarajiwa kupokea tuzo maalum ya ubunifu (Innovator Award) kutokana na mchango wake mkubwa katika muziki huku mwanamuziki Taylor Swift akiongoza kwa kuingia katika vipengele vingi vya tuzo hizo (nominations).
Kwa mujibu wa waandaaji wa tuzo hizo, Ludacris hatakuwa tu mtangazaji, bali pia atatumbuiza jukwaani pamoja na kupokea tuzo maalum ya heshima kwa mchango wake mkubwa katika muziki.
Mbali na Ludacris, wasanii wengine wakubwa watakaotumbuiza ni pamoja na Lainey Wilson na RAYE, huku kukitarajiwa kuwepo kwa ushirikiano wa kipekee wa kundi la TLC, Salt-N-Pepa na En Vogue kwa mara ya kwanza jukwaani.
Uaiku wa tuzo hizo umepangwa kuwa na burudani ya hali ya juu, zikijumuisha maonesho makubwa, tuzo za heshima na mambo mbalimbali ya kushangaza kwa wanamuziki na mashabiki kwa ujumla




