Liverpool yashusha ‘Pacha’ wa Marmoush

LIVERPOOL, Mabingwa wa Ligi kuu ya England Liverpool wamemsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa Hugo Ekitike kutoka Eintracht Frankfurt, kwa dau linaloripotiwa kuwa na thamani ya pauni milioni 69 pamoja na nyongeza.
Ekitike ni mchezaji wa pili kwa bei ghali zaidi kusajiliwa Liverpool kwenye dirisha hili la usajili baada ya mabingwa hao wa Premier League kumsajili kiungo wa kati wa Ujerumani Florian Wirtz, ambaye pia anaweza kucheza kama winga au mshambuliaji kwa dau lililoweka rekodi la pauni milioni 100 pamoja na nyongeza.
“Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 amekamilisha vipimo vya afya na kukubaliana masuala binafsi na Reds, na kumruhusu kusafiri hadi Hong Kong kuungana na wachezaji wenzake katika ziara yao ya kujiandaa na msimu ujao barani Asia baadaye wiki hii,” Liverpool imesema katika taarifa ya utambulisho wa mchezaji huyo.
Ekitike, Mchezaji wa zamani wa Paris St Germain amekuwa msimu wa aina yake akifunga mabao 15 kwenye Bundesliga katika mechi 33 alizoichezea Frankfurt na kuchangia mabao manne katika kampeni yao ya Europa League
Raia huyo wa Ufaransa ambaye alicheza mechi yake ya kwanza katika klabu ya Stade de Reims alijiunga na PSG kwa mkopo mwaka 2022, na kucheza mechi 25 za Ligue 1 akifanikiwa kushinda taji hilo Alikwenda kwa mkopo Frankfurt mwaka 2023 kabla ya kufanya uhamisho huo kuwa wa kudumu mwaka mmoja baadaye.