EPL

Liverpool kurudisha kiwewe United?

LONDON: KOCHA wa Manchester United, Ruben Amorim, huenda akarejea tena kwenye shinikizo kubwa la Ligi Kuu ya England Jumapili wakati klabu yake itakaposafiri hadi viunga vya Anfield kuvaana na Liverpool, licha ya kupata ahueni kidogo wakati wa mapumziko ya michezo ya kimataifa kufuatia kuungwa mkono na mmoja wa wamiliki wa klabu, Sir Jim Ratcliffe.

Ratcliffe amependekeza kwamba Amorim, ambaye yuko chini ya presha kubwa kutokana na matokeo mabovu ya United apewe muda wa miaka mitatu kamili ya mkataba wake ili kuibadili hali ya United licha ya ukosefu wa dalili zinazothibitisha kuwa Mreno huyo ana uwezo wa kuirejesha timu hiyo kwenye ubora wake.

Ushindi dhidi ya mabingwa watetezi, ambao wamepata matokeo mabovu mechi zao tatu za mwisho, utamaanisha United kushinda michezo miwili mfululizo ya ligi kwa mara ya kwanza tangu Amorim alipokabidhiwa timu hiyo takribani mwaka mmoja uliopita.

Hata hivyo, kipigo katika uwanja wa Anfield, ambao unajulikana kwa presha ya aina yake, kunaweza kutikisa imani ya Ratcliffe, ambaye alimpendekeza Amorim kufuatia kufutwa kazi kwa Erik ten Hag, lakini hadi sasa amepata ushindi wa mechi 10 pekee kati ya michezo 34 ya EPL.

Ratcliffe amelinganisha mwanzo wa Amorim na ule wa kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, aliyekuwa na kipindi kigumu mwanzoni kabla ya kuibadilisha Arsenal kuwa mshindani wa kudumu wa taji kwa takriban miaka minne hoja iliyozua mijadala miongoni mwa wadau wa soka akiwemo beki wa zamani wa United, Rio Ferdinand, ambaye kupitia podikasti yake ya Rio Ferdinand Presents ambaye amesema haoni mantiki ya ulinganifu huo.

Related Articles

Back to top button