Ligi Kuu

Ligi Kuu kurejea kesho baada ya AFCON

DAR ES SALAAM: LIGI Kuu Tanzania Bara inarejea rasmi kesho baada ya mapumziko yaliyotokana na majukumu ya timu ya Taifa katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) pamoja na kukamilika kwa mashindano ya Kombe la Mapinduzi.

Ratiba ya kurejea kwa ligi hiyo inaanza kesho kwa mchezo wa kusisimua kati ya Dodoma Jiji FC na Singida Black Stars, mechi inayotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na mwenendo wa timu hizo katika msimu huu.

Azam FC itawakabili Coastal Union keshokutwa, ikiwa ni fursa kwa klabu hiyo kupunguza pengo la pointi dhidi ya wapinzani wake wa juu ya msimamo wa ligi.

Kurejea kwa ligi kunakuja baada ya wachezaji wengi wa klabu mbalimbali kuwa katika majukumu ya kuwakilisha mataifa yao kwenye fainali za AFCON, hali iliyosababisha kusitishwa kwa ligi kwa muda, sambamba na kukamilika kwa mashindano ya Kombe la Mapinduzi yaliyomalizika hivi karibuni.

Katika michezo mingine ya mzunguko huu, mabingwa watetezi Yanga watashuka uwanjani Jumatatu wakiwakaribisha Mashujaa FC, huku wapinzani wao wa jadi Simba SC wakicheza Jumapili dhidi ya Mtibwa Sugar, mechi inayotarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi.

Kurejea kwa Ligi Kuu kunatarajiwa kuamsha upya ushindani mkali wa ubingwa pamoja na mapambano ya kuwania nafasi za juu na kuepuka kushuka daraja, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona timu zao zikiendelea na mbio za msimu.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button