Ligi KuuNyumbani

Ligi Kuu Bara yaanza na moto

AGOSTI 19 kulianza mechi za raundi ya pili za Ligi Kuu ya NBC baada ya katikati ya wiki hii kupigwa mechi za raundi ya kwanza zikiwa na matokeo ya sare ya mechi moja tu.

Baada ya mwezi mzima wa kujipanga, kuweka kambi huku na huko na tambo mbalimbali, hatimaye ligi imerejea na sasa majibu yameanza kutoka kuhusu vikosi vya timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo, maarufu kwa sasa ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Kwa jicho la tofauti kila timu imeonesha ilichonacho kwenye dakika 90 za mechi zao za kwanza na angalau kuonesha taswira ya vikosi vyao kwa msimu huu wa 2022/23. Mabingwa watetezi, Yanga walianza kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania katika mechi ngumu na yenye kuvutia.

Yanga ambao walimaliza ligi bila kupoteza mchezo msimu uliopita, wameonekana kuendelea kuwa imara kwa maana ya nafasi nyingi za kufunga mabao walizotengeneza ingawa walipata idadi ndogo ya mabao.

Mshambuliaji wao hatari, Fiston Mayele ameendelea kuzifumania nyavu kama ilivyokuwa msimu uliopita. Bernard Morrison aliyesajiliwa msimu huu naye ameonesha ubora wake kiasi cha kutoa pasi ya bao la pili na la ushindi.

Uwepo wa wachezaji wapya kama beki wa kushoto, Joyce Lomalisa, viungo Stephane Aziz Ki, Gael Bigirimana na mshambuliaji Lazarous Kambole kumeongeza upana wa kikosi hicho na kuonesha jinsi gani wamepania kulitawala soka la Tanzania kwa misimu kadhaa zaidi.

Unaweza kusema Yanga imeanza ilipoishia msimu uliopita, kwani tayari wametetea taji lao la Ngao ya Jamii kwa kuifunga Simba mabao 2-1.

Ndiyo, hii ni mechi ya pili mfululizo, Yanga inapata matokeo ya 2-1 na hutanguliwa kufungwa wao lakini mwisho wanaondoka na ushindi, hii ndiyo maana halisi ya kikosi kipana na chenye kuhitaji mafanikio zaidi.

Watani wa jadi wa Yanga, Simba ambayo imeanza ligi kwa ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Geita Gold wameonesha kutaka kurejesha ufalme wao nchini kutokana na kasi ya uchu wa utafutaji mabao iliyokuwa nao kwenye mchezo wao huo wa kwanza.

Uwepo wa washambuliaji wenye kasi kama Pape Sakho, Peter Banda, Moses Phiri na Augustine Okrah unawaweka kwenye wakati mgumu wapinzani wanaokutana nao ingawa kikosi hicho kinakosa utulivu kwenye eneo la kiungo.

Mara kadhaa kulipotea mipira kwenye eneo hilo bila ya sababu za msingi au kukosekana kwa mawasiliano.

Kocha Zoran Maki akimaliza kutibu tatizo hilo, pia amtafute mapema mno namba tisa wake wa kudumu kwenye kikosi hicho ili afaidi vizuri matunda ya wakina Sakho kwenye eneo la mwisho la kufunga mabao.

Phiri hatulii kwenye boksi, mipira mingi inaishia kwa mabeki. Mshambuliaji mpya Dejan Georgijevic ‘Mzungu’ bado kazi yake haijalishawishi sawasawa benchi na hata umma unaomfuatilia.

Habibu Kyombo yupo kwenye presha ya timu kubwa na kongwe, lakini hapaswi kuiendekeza hiyo presha, afanye kazi yake iliyomfanya asaini Simba, mambo mengine amwachie kocha.

Zoran akifanikiwa kurejesha makali ya nahodha wake, John Bocco au kuwaweka sawa hao washambuliaji wengine, basi atafaidika mno na Simba itanukia mabao mengi msimu huu. Tusubiri.

Upande wa matajiri wa jiji, Azam FC ni kama vile wamepania na wanautaka ubingwa waliouchukua mara ya mwisho 2013/14. Usajili wa wachezaji tisa wapya na kiwango walichoonesha wakati wanainyoosha Kagera Sugar mabao 2-1 kilitosha kutambulisha uwepo kwa sauti kubwa.

Ukiachana na nafasi nyingine uwanjani ambazo wachezaji hao wapya wameonesha kumudu majukumu yao lakini pia safari hii timu hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutibu tatizo la golikipa.

Kipa wao Mcomoro, Ali Ahamada alifanya kazi kubwa na ya ziada hata ilipotokea Kagera wametutumka na wanataka kuchomoa bao, yeye alipambana kiume kuhakikisha hakiharibiki kitu na Azam inaondoka na pointi tatu.

Uwepo wa wachezaji wapya tisa ndani ya kikosi ambao wote wanafaa kuanza ni mtihani mkubwa ambao kocha Abdihamid Moallin ameanza kuufanya kwa mafanikio makubwa akijitahidi kuchanganya wachezaji wa zamani na sasa na matokeo yameanza kuonekana kwa kandanda safi wanaloonesha.

Timu hizi zote tatu msimu ujao zitaiwakilisha nchi kwenye michuano ya klabu Afrika na usajili wao unatia moyo kuelekea kwenye michuano hiyo, wachezaji waliowachukua ni miongoni mwa sura za michuano hiyo, tutarajie makubwa.

Timu nyingine inayoungana na vigogo hao kimataifa ni Geita Gold ambayo imefungwa mabao 3-0 na Simba.

Kuhusu usajili Geita iko vizuri japo hawajaegemea sana kwa wachezaji wa kimataifa lakini beki wa kushoto, Yahya Mbegu waliyemchukua kutoka Polisi Tanzania ameendelea kusimama kwenye ubora wake.

Oscar Masai aliyekuja kuziba pengo la Juma Nyosso naye ameonesha ukomavu kama ilivyokuwa kwa George Wawa na walionesha kutafuta kitu isipokuwa waliangushwa na mipango yao mbele ya Simba.

George Mpole ambaye ni mfungaji bora msimu uliopita hajamaliza, ana kitu mguuni mwake na inawezekana mazingira ya ugumu wa mechi yalimkwamisha kuanza balaa lake juzi. Kocha Fred Minziro atazame mpango mbadala kwa Mpole kwani anafahamika ndiyo silaha kubwa ya Geita akishirikiana na Ayoub Lyanga.

Abadili kitu ili awachanganye wapinzani na wasikariri kuwa atapita wapi ili apate mabao ya ushindi. Wakati vigogo wakitoa taswira yao, timu iliyopanda daraja msimu huu, Singida Big Stars iliipiga Tanzania Prisons bao 1-0 lililowekwa kimiani na Mbrazil, Petreson Cruz kwa ‘tik-taka’ safi.

Cruz na mwenzake Dario Junior ni miongoni mwa sajili zinazotikisa nchini kwa viwango walivyonavyo tangu kwenye mechi zao za kujiandaa na msimu mpaka kwenye ligi. Kabla ya kufika mbali, Singida imesajili mno, ina mastaa wa kutosha na kila mmoja anasubiri matokeo yao mwisho wa msimu.

Hata kocha waliyenaye, Mholanzi Hans van Der Pluijm ni mzoefu na soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla hivyo anajua nini cha kufanya.

Kipa Metacha Mnata, Meddie Kagere, Abdul Mangalo, Amissi Tambwe, Deus Kaseke, Said Ndemla, Juma Abdul, Pascal Wawa, Asamoah Gyan na wengine wengi ni uthibitisho kuwa wana jambo lao msimu huu, tuendelee kuwatazama.

Ihefu iliyopanda na Singida, iliangukia pua ikifungwa bao 1-0 na Ruvu Shooting. Ihefu iko sawa kuanzia wachezaji wazoefu mpaka kocha wao, Zuberi Katwila ni mtu wa soka hasa. Kwenye kikosi chao imewavuta Nyosso, Obrey Chirwa, Peter Mwalyanzi, Never Tigere, Said Makapu, Papi Tshishimbi na wengine.

Ingawa Ihefu ina historia mbaya ilipopanda mara ya mwisho na kushuka msimu huo huo lakini binafsi nawapa nafasi ya kuwaona tena.

Wana kitu kwa namna wanavyopanga mashambulizi yao na hata wanavyozuia kwa heshima ya soka, yawezekana wamekuwa na mwanzo mbaya lakini watajifunza kitu na pengine kukaa sawa kabla mambo hayajawa magumu zaidi.

Ruvu inaonekana haitaki iwatokee yaliyowatokea msimu uliopita kupambana isimalize nafasi ya kucheza ‘play-off’ kuwania isishuke daraja ndiyo maana safari hii mapema imezoa pointi tatu asubuhi tu.

Ni kama Mtibwa Sugar ilivyokomaa kwa Namungo kwa sare ya mabao 2-2. Mtibwa nayo chupuchupu ishuke daraja kama si kucheza mechi hizo za mtoano zilizoibakisha timu hiyo Ligi Kuu ya NBC. Mchezo wao ulikuwa mgumu kutokana na ubora iliokuwa nao Namungo.

Namungo haijabadilika sana, imeongeza sura chache zenye uzoefu wa ligi kama kipa Deo Munishi ‘Dida’, Hassan Kabunda, Pius Buswita na wengine wanaoungana na wachezaji waandamizi kama Reliants Lusajo ambaye tayari alishaweka kambani bao mbili na kuamsha morali ya timu hiyo.

Timu hiyo kutoka Lindi ni miongoni mwa timu zenye ubora zinazowekwa daraja la kati kiushindani nchini na kuna muda ni tishio mbele ya vigogo, bado wataonesha makubwa msimu huu.

Washindi wa pili wa Kombe la FA, Coastal Union wameanza vyema kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC. Kwa jicho la ufundi, timu hizi hazijapishana sana kiuchezaji ingawa vijana wa KMC walichangamka na kucheza soka safi dhidi ya wapinzani wao.

Timu zote zinahitaji kuongeza kitu kwenye vikosi vyao kwa ajili ya kuongeza ushindani unaoonekana mgumu zaidi msimu huu kutokana na kila timu ilivyojipanga.

Mbeya City haijabadilika vya kutosha, isipokuwa ni kama imezibuka na kutembeza kichapo cha mabao 3-1 kwa Dodoma Jiji, timu ambayo ilionesha kiwango kizuri misimu miwili iliyodumu kwenye ligi.

Ni Mbeya City na Simba pekee ndio waliofunga idadi kubwa ya mabao mpaka sasa, ni ngumu kuiweka City kwenye daraja moja na Simba lakini imefanya kitu, wengi wanahisi ni nguvu ya soda kutokana na mwendo wao katika misimu ya hivi karibuni.

Lakini kuthibitisha nguvu ya soda au kama kweli wapo ‘siriaz’ ni kuendelea na moto wao kwenye mechi zinazofuata.

Itoshe kusema ligi imeanza na moto na kila timu inafanya yake kujitetea ili iendelee kutesa kwenye Ligi Kuu kutokana na ukweli wa upatikanaji wa mapato ulioanza kukaa sawa, ushindani bora na kujitangaza zaidi Afrika.

Wito kidogo kwa wasimamizi wa ligi, Bodi ya Ligi (TPLB), Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na waamuzi kwa ujumla kutengeneza mazingira rafiki ya ushidani ulioonekana mapema.

Kusiwepo kwa maamuzi yenye utata wa makusudi au kujificha nyuma ya kivuli cha makosa ya kibinadamu, tutakuwa tunabebana bure huku tukijirudisha nyuma, makandokando ya mikataba ya kiholela kama tulivyoshuhudia msimu uliopita isiwepo tena ili angalau tufurahie soka letu.

Mkanganyiko wa ratiba na kuweka viporo visivyo na maana pia visiwepo ili kuwe na weledi angalau na malalamiko yapungue, tuache timu zijihukumu zenyewe kwa usajili na mipango yao, wasisaidiwe kuvunjwa moyo au kutibuliwa mambo. Tuache soka lichukue nafasi yake halisi.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button