“Kutwaa makombe sio kufanikiwa” – Arteta

LONDON: MENEJA wa Arsenal Mikel Arteta amewapongeza mahasimu wao wa London Kaskazini Tottenham Hotspur kwa kushinda taji la Europa League usiku wa Jumatano, lakini akasisitiza kwamba timu ikishinda kombe haipaswi kujiona imefanikiwa.
Arteta amewaambia waandishi wa Habari kuelekea mchezo wao wa mwisho wa Ligi kuu ya England dhidi ya Southampton ambayo tayari imeshuka daraja jioni ya Jumapili, kuwa mafanikio ndani ya msimu hayawezi kupimwa kwa kuwa timu imetwaa ubingwa bali njia na aina ya uchezaji kuelekea ubingwa huo.
“Wao ni mabingwa (wa Europa) na unapofikiria hilo lazima ufanye mambo mengi kwa usahihi mkubwa. Nadhani wamepitia msimu wenye vikwazo na matatizo mengi. Lakini hatimae mwishoni wana kitu wamepata… wana wakati mzuri sana, nawapongeza” Arteta alisema.
Alipoulizwa katika ni timu ipi kati ya timu yake (Arsenal) na Tottenham imekuwa na msimu mzuri zaidi, Arteta alikwepa kujibu moja kwa moja akisema hapendi kulinganisha timu yake na timu nyingine kimafanikio ya msimu huu hasa kama timu hiyo ni Tottenham na anapenda kujitathmini yeye mwenyewe bila kuangalia mtu mwingine ananini.
Mhispania huyo, ambaye aliiongoza Arsenal katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa alisema timu haipaswi kuhukumiwa kwa hesabu ya vikombe kwa msimu, akitoa mfano wa timu yake, ambayo haijawahi kushinda Ligi ya Mabingwa na haijabeba taji la Ligi Kuu tangu msimu wa 2003-04 lakini ni miongoni mwa timu bora msimu huu.
“Furaha halisi ni ipi basi? Kwa sababu lazima tujichambue … tumeshindwa kwa miaka 20 kwenye Ligi Kuu na hatuna lolote katika historia yetu yote kwenye Ligi ya Mabingwa. Basi Sisi ni nani? ‘Brand’ yetu iko wapi, klabu yetu iko wapi … iko wapi heshima yetu, ni upi uchezaji wetu? Ziko wapi nyakati ambazo tulikuwa pamoja na watu wetu?” Arteta alisema.