
MSHAMBULIAJI wa Polisi Tanzania, Vitalis Mayanga amesema siri ya ushindi wa timu hiyo dhidi ya Namungo katika mchezo wa Ligi Kuu Oktoba 19 ni wachezaji kupambana kwa ajili ya klabu.
Akizungumza na Spotileo mshambuliaji huyo amesema pamoja na changamoto wanazozipitia za kutokuwa na kocha mkuu lakini walipanga kupambana ili kujiondoa kwenye nafasi mbaya katika msimamo wa ligi.
“Ushindi wetu umetokana na jitihada na bidii zetu wenyewe wachezaji. Kabla ya mchezo tulikaa na kukubaliana kupambana nashukuru tumetimiza lengo,” amesema Mayanga.
Mshambuliaji huyo amesema bado wataendelea kupambana katika mechi zijazo na dhamira ni kuhakikisha wanapanda kwenye nafasi za juu.
Kwa ushindi huo wa kwanza wa ligi msimu huu Polisi Tanzania wanashika nafasi ya 15 kwenye msimamo ikiwa na pointi 5 baada michezo 7.