Kuogelea kuwakilisha mashindano ya Africa

CHAMA cha Kuogelea Tanzania (TSA) kimetaja wachezaji 14 watakaojiandaa na mashindano ya vijana ya kuogelea ya Afrika yatakayofanyika kuanzia Aprili 30 hadi Mei 3, mwaka huu nchini Misri.
Kwa mujibu wa taarifa ya Msemaji wa TSA Sebastian Kolowa leo Machi 3,2025 kwa vyombo vya habari, timu imeshaanza maandalizi ya michuano hiyo kuhakikisha inakwenda kushiriki na kufanya vizuri.
“Kati ya waogeleaji hao, saba ni wanaume na wengine saba ni wanawake. Uchaguzi wa kikosi umetokana na mashindano mbalimbali yaliyopita ikiwemo iliyofanyika wiki mbili zilizopita,”amesema.
Amesema: “Tunaendelea kuwaomba Watanzania waendelee kuiombea timu hii ili iende ikawakilishe vizuri,”.
Waogeleaji hao ni Romeo Mwaipasi, Aryan Bhatt, Mark Tibazarwa, Austin Okore, Christian Fernandes, Enrico Baretto, Sahal Haarunani. Wengine ni Filbertha Demello, Lina Goyayi, Bridget Heep, Natalia Ladha, Amylia Chali, Aliyana Kachra na Aminaz Kachra.
Kolowa amesema timu itaondoka Tanzania Aprili 28 na kurudi Mei 4.