Kocha Yanga alia ugumu wa ratiba

DAR ES SALAAM : KOCHA Mkuu wa Yanga, Pedro Gonçalves, amesema ushindi walioupata haukuwa rahisi licha ya matokeo kuonekana makubwa, akisisitiza umuhimu wa umoja wa kikosi kizima pamoja na mchango wa wachezaji wa akiba.
Kauli yake hiyo imekuja baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa jana kwenye Uwanja wa KMC Dar es Salaam.
Amesema kuwa mchezo ulikuwa na ushindani mkubwa hadi walipopata bao la kwanza lililotokana na mpango walioufanyia kazi mazoezini.
“Haikuwa mechi rahisi, ilikuwa ngumu sana. Kabla ya kufika kwenye matokeo makubwa kulikuwa na ushindani mkali. Tulipata bao zuri kupitia kitu tulichokuwa tunakifanyia kazi mazoezini,” amesema.
Ameongeza kuwa kipindi cha pili wapinzani waliongeza presha, hali iliyowalazimu kuwataka wachezaji wake kubaki makini na kudhibiti mchezo, huku akiwapongeza wachezaji waliotoka benchi kwa kubadili mwendo wa mechi.
“Sio wachezaji 11 pekee, hata walioko benchi ni sehemu ya mchezo. Walioingia walifanya kazi nzuri sana.”
Kocha huyo pia alizungumzia ratiba ngumu ya mechi walizonazo, akibainisha kuwa uchovu umeonekana kwa baadhi ya wachezaji kutokana na kucheza bila kupata hata saa 72 za kupumzika pamoja na safari za mara kwa mara.
Kocha huyo aliwashukuru mashabiki wa Yanga kwa sapoti yao, akiwataja kama mchezaji wa 12 na kusisitiza kuwa ndani ya klabu hiyo kila mtu ni familia.
Kikosi cha Yanga tayari kimeondoka leo kuelekea Zanzibar kwa ajili ya mchezo wa watani wa jadi dhidi ya Simba utakaochezwa Jumapili.




