KMC yapumua baada ya ushindi wa pili
DAR ES SALAAM: KMC FC hatimaye imepata ahueni baada ya kuibuka na ushindi wake wa pili wa mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, ikiifunga Mashujaa FC katika mchezo wa raundi ya 13, ushindi uliopatikana kupitia bao la mpira wa adhabu lililofungwa na Daruweshi Saliboko jana.
Ushindi huo ni wa pili kwa KMC baada ya kucheza michezo 11 mfululizo bila kupata ushindi, hali iliyokuwa imeiweka timu hiyo kwenye presha kubwa ya kushuka daraja.
Awali, ushindi mwingine pekee wa KMC msimu huu ulikuwa katika raundi ya kwanza walipoifunga Dodoma Jiji bao 1-0, kabla ya kuingia kwenye mlolongo mrefu wa matokeo duni.
Licha ya ushindi wa jana, KMC bado inashikilia mkia wa msimamo wa ligi ikiwa na pointi nane baada ya kucheza michezo 13, hali inayoonesha kuwa bado ina safari ndefu ya kupambana ili kujinasua katika eneo la hatari.
Hata hivyo, dalili za mabadiliko zimeanza kuonekana, ambapo maboresho machache yaliyofanywa na klabu hiyo katika dirisha dogo la usajili yanaonekana kuanza kuleta matokeo chanya, hasa katika eneo la uchezeshaji wa mpira na nidhamu ya timu.
Endapo KMC itaendelea kujipanga na kutumia vyema fursa katika michezo ijayo, ushindi huo unaweza kuwa mwanzo wa kurejea kwenye mstari, ingawa changamoto ya kuondoka mkiani bado ni kubwa.
Mwisho




