Kizuguto kuratibu mchezo wa Nigeria, Gabon

DAR ES SALAAM: SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) limemteua Meneja wa Mashindano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, kuwa Mratibu Mkuu wa michezo ya nusu fainali na fainali ya hatua za awali za kufuzu Kombe la Dunia Kanda ya Afrika
Kizuguto anatarajiwa kusimamia michezo hiyo mikubwa itakayowakutanisha Nigeria dhidi ya Gabon katika nusu fainali, pamoja na mchezo wa fainali utakaochezwa baadaye.
Mechi hizo zimepangwa kufanyika jijini Rabat, Morocco mnamo Novemba 13 na Novemba 16, 2025.
Uteuzi huo umetangazwa na TFF kama sehemu ya kutambua mchango na uwezo wa watendaji wa Tanzania katika kushiriki kwenye ngazi za juu za mpira wa miguu kimataifa.
Kizuguto, ambaye kwa kipindi cha miaka ya karibuni amekuwa sehemu ya waandaaji na wasimamizi wa mashindano mbalimbali ya kimataifa kupitia CAF na FIFA, anazidi kuiweka Tanzania katika ramani ya viongozi wanaotegemewa ndani ya soka la Afrika.




