Kitayosce, Fountain gate zafungiwa kusajili

KLABU za Kitayosce iliyopo Ligi Kuu Tanzania Bara na Fountain Gate inayocheza Ligi ya Championship zimefungiwa kusajili wachezaji.
Taarifa ya Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) imesema uamuzi huo umefanywa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu(FIFA) baada ya Kocha Ahmed El Faramawy Yousef Mostafa Soliman kushinda kesi za madai dhidi ya klabu hizo.
“Kocha huyo raia wa Misri ambaye alizifundisha timu hizo kwa nyakati tofauti alifungua kesi FIFA akipinga kuvunjiwa mikataba kinyume cha taratibu,” imesema TFF.
Aidha taarifa hiyo imesema: “Baada ya Soliman kushinda kesi, klabu hizo zilitakiwa ziwe zimemlipa ndani ya siku 45 tangu uamuzi huo ulipotolewa, lakini hazikutekeleza hukumu hizo.”
Wakati FIFA inazifungia klabu hizo kufanya uhamisho wa wachezaji wa kimataifa, TFF imezifungia kufanya uhamisho wa ndani.