Kipute fainali Europa conference leo

WAPIGA Nyundo wa London, klabu ya West Ham United inajitupa dimbani leo kuikabili Fiorentina ya Italia katika fainali ya Ligi ya Europa Conference huku wapiga nyundo hao wakisaka kushinda taji la kwanza kubwa kwa kipindi cha miaka 43 iliyopita.
Kuna habari kwamba hadi elfu-20 mashabiki wa West Ham watakuwa mji mkuu wa Jamhuri ya Czech, Prague licha ya klabu hiyo kupata tiketi 4,890 kuingia kwenye uwanja wa Fortuna wenye uwezo wa kupokea watazamaji 19, 370 tu.
Huo ni mchezo wa 15 wa West Ham barani Ulaya kwa msimu huu baada ya kuanza kampeni kuwania taji la Ligi ya Europa Conference katika raundi ya mtoano August 18, 2022.
“Tuna furaha kubwa kuwa katika fainali. Ni mafanikio makubwa kwa klabu, lakini sasa ni kuhusu kwenda na kuyashinda. Ni mchezo maalumu,” amesema Kocha Mkuu wa Wapiga Nyundo, David Moyes.
Kwa upande mwingine Fiorentina imemaliza nafasi ya nane Ligi Kuu ya Italia, Serie A na haijashinda taji lolote kubwa la ulaya tangu ilipotwa Kombe la Washindi barani Ulaya msimu wa 1960-61.
Timu hiyo inayonolewa na Vincenzo Italiano imepoteza mechi tatu za Ligi ya Europa Conference msimu huu lakini imetinga fainali kuikabili West Ham.
“Ni msimu wangu wa kwanza barani Ulaya na nimeridhika sana kufika fainali. Hatua hii ya fainali itabaki nasi siku zote lakini sasa tuna dhamira ya kukamilisha,” amesema Italiano.
Huu ni msimu wa pili wa Ligi ya Europa Conference na ni michuano ya tatu ya klabu barani Ulaya baada ya Ligi ya Mabingwa na Ligi ya Europa.
Roma ilishinda fainali ya uzinduzi wa Ligi ya Europa Conference kwa kuifunga Fenenoord msimu wa 2021/22.