Masumbwi

Kibwana, Nkane nusura wazichape wakitambiana

WACHEZAJI wa Yanga, Kibwana Shomari na Denis Nkane, nusura wazichape mbele ya waandishi wa habari baada ya kutambiana kwa maneno makali kuelekea pambano la ngumi la Dar Boxing Derby litakalofanyika Julai 26, mwaka huu, katika viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam.

Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo kwenye ofisi za Azam Media, Kibwana alionekana mwenye kujiamini huku akimtupia maneno mazito mpinzani wake, akimtaja Nkane kama “mtoto wa maneno mengi” na kuwataka wakazi wa Buza, alikotoka Nkane, kujiandaa kwa tukio la kusikitisha.

“Huyu kijana amekuwa akiniposti vibaya mitandaoni, kwa hiyo nimejiandaa na ngumi inayoitwa ‘kata funua’, yaani nikate nimfunue. Sitaki maneno, nataka nimfundishe adabu,” alisema Kibwana, ambaye atakuwa kambini kwa Twaha Kiduku mkoani Morogoro.

Kwa upande wake, Nkane hakubaki kimya. Akiwa na mbwembwe, alijibu kwa maneno ya kejeli akidai Kibwana “ameyakanyaga” na kwamba anaandaliwa kwa ngumi ijulikanayo kama “jiwe”, huku akisema mizimu ya kwao “inahitaji damu”.

“Kama sheria ingeruhusu, tungeanza kuzichapa hapa,” alisema Nkane, ambaye kwa sasa yuko kwenye kambi ya bondia Mfaume Mfaume.

Promota wa pambano hilo, Seleman Semunyu kutoka Peak Time Promotion, alieleza kuwa maandalizi ya pambano hilo yako vizuri, huku akizishukuru klabu ya Yanga, wachezaji wake na wadhamini waliosimama nao.

“Nawashukuru Yanga kwa kuridhia wazo hili. Tunaamini mashabiki na wanachama wa Yanga watatuunga mkono. Euromax wameanza kutuunga mkono, tunawahamasisha na wadhamini wengine waendelee kuja mbele,” alisema Semunyu.

Kwa mujibu wa Semunyu, mpaka sasa hakuna bondia aliyejiondoa kwa sababu ya majeraha na mashabiki wanatarajia kuona burudani ya hali ya juu.

Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe, alisema klabu hiyo imekuwa mstari wa mbele kuendeleza vipaji mbalimbali, si katika mpira wa miguu pekee bali pia kwenye michezo mingine.

“Sio mara ya kwanza kushirikiana na Peak Time. Tuliwahi kutoa semina ya mitandao ya kijamii kwa mabondia na tuna bondia hata kwenye nembo yetu. Hili ni jambo jema kwa klabu yetu na vijana wetu,” alisema Kamwe.

Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Euromax, Peter Michael, alisema wamefurahishwa na mchango wa Peak Time katika kukuza mchezo wa ngumi nchini na kwamba anaamini pambano litakuwa la kuvutia na wao kama Euromax watakuwa sehemu ya maendeleo haya ya michezo.

Related Articles

Back to top button