Ligi Kuu

Kibu Denis atupa jiwe gizani

DAR ES SALAAM: MSHAMBULIAJI wa Simba SC, Kibu Denis amesema kuwa wanahitaji kuwa makini na kujituma zaidi katika michezo ya mwisho ya msimu huu ili kuhakikisha wanavuna pointi zote muhimu, kwani ushindi katika hatua hii si tu muhimu kwa timu bali pia unagusa hisia za mashabiki wengi.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya Ken Gold, Kibu amesema kwamba licha ya ushindi wa mabao 5-0 walioupata kwenye Uwanja wa Al Hassan Mwinyi, Tabora, mchezo huo haukuwa mwepesi kama wengi walivyotarajia.

Amesema changamoto kubwa walikumbana nayo ilikuwa kucheza dhidi ya timu ambayo tayari imeshashuka daraja, hivyo haikuwa na presha ya kutafuta matokeo, tofauti na wao ambao wanapambana kufukuzia taji la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Hizi mechi za mwisho wa msimu zinakuwa na ugumu wao. Unapokutana na timu kama Ken Gold, ambayo haina tena cha kupoteza, mara nyingi zinacheza kwa uhuru mkubwa, lakini sisi tunahitaji pointi tatu kwa gharama yoyote, hivyo presha iko juu zaidi kwetu,” amesema Kibu.

Ameongeza kuwa mafanikio ya mchezo huo yalitokana na kupata bao la mapema liliwasaidia kutuliza presha na kuanza kuendesha mchezo kwa utulivu, jambo lililowasaidia kupata ushindi wa kishindo.

“Mpango wetu ulikuwa kupata bao mapema, tulifanikiwa. Tulipata nafasi, tukazitumia vizuri, na hilo lilitufanya kujiamini zaidi hadi mwisho wa mchezo,” ameongeza mshambuliaji huyo.

Kibu amesema kwa sasa akili na nguvu zao zote wamezielekeza kwenye mchezo unaofuata dhidi ya Kagera Sugar, ambao nao tayari wameshuka daraja, lakini bado wanapaswa kuwachukulia kwa uzito mkubwa.

Simba wanatarajiwa kushuka tena dimbani Jumapili, Juni 22, katika Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam, kumenyana na Kagera Sugar katika mchezo wa mwisho wa ligi kwao msimu huu kabla ya pambano lao la Kariakoo Derby mchezo wa kiporo, utakaochezwa Jumatano Juni 25.

Related Articles

Back to top button