Burudani

Khadija Kopa awapasha ‘Content Creators’

DAR ES SALAAM: MSANII nguli wa muziki wa taarab nchini, Khadija Kopa, amewataka watengeneza maudhui na wanahabari wa mitandaoni kuacha kuangazia tu mabaya ya wasanii na badala yake wawasaidie kwa kuwashauri na kuwaelekeza mambo ya kufanya ili kuboresha maisha yao.

Akizungumza na Spoti Leo, Malkia Kopa amesema kuwa jukumu lake katika programu anayoshiriki ni kutoa elimu kwa vijana, siyo kufuatilia au kusambaza habari za umbea mtandaoni.

“Nipo kwenye kipindi cha Wapea, lakini mimi sio mmbea. Niko pale kuwaelimisha wanangu wa kike na wa kiume juu ya kile wanachopaswa kufanya,” amesema.

Amesisitiza kuwa watoa maudhui mitandaoni wanapaswa kujenga jamii, siyo kueneza tu taarifa hasi zinazohusu maisha ya watu maarufu.

“Wanaofanya umbea mitandaoni, wakizungumzia maisha ya watu, msiwaseme tu kwa mabaya. Elimisheni pia ni kitu gani sahihi wanachopaswa kufanya,” amesema.

Malkia Kopa ameongeza kuwa habari mbaya kusambaa ni rahisi, lakini umuhimu unakuja pale ambapo mtoa taarifa anamwonyesha mtu njia sahihi ya kuboresha maisha yake.

“Unapotangaza mabaya ya mtu fulani, hayo yanasambaa haraka. Lakini je, umemwambia alipaswa kufanya nini? Tuwape mwongozo, wasipofuata ndipo tuseme: ‘Tuliwaambia’.”

“Nipo kwenye kipindi cha tashtiti sio kwa umbea nipo ili kuwaelimisha na kuwafundusha wasanii na jamii kwa ujumla kama mzazi vitu vipi wanapaswa kufanya na sio kuwasimanga na kuwasema vibaya kwa kuwa ukimsema hujamsaidia bado inapaswa kumwambia nini chakufanya.”amesema Malkia Khadija

Related Articles

Back to top button