Tetesi

Kane mbadala wa Benzema

MSHAMBULIAJI Harry Kane wa Tottenham Hotspur ni chaguo la kwanza katika Klabu ya Real Madrid kuchukua nafasi ya Karim Benzema iwapo mfaransa huyo ataamua kuhamia klabu ya Al-Ittihad ya Saudi Arabia, mtandao wa michezo wa 90min umesema.

Kwa muda mrefu Madrid imekuwa ikivutiwa na Kane lakini haijatarajia kuhitaji kusajili mbadala wa Benzema hadi majira yajayo ya joto kwani alikuwa amekubali vipengele vya kusalia katika mji mkuu wa Hispania kwa miezi 12 zaidi.

Hata hivyo, dili la Benzema halijasainiwa na sasa anaeleweka kuwa anakaribia kukubali mkataba wa miaka miwili kujiunga na Al-Ittihad ya Ligi Kuu ya Saudi Arabia.

Kwa mujibu wa 90min sasa timu ya usajili ya Real ikiongozwa na Juni Calafat inapanga mbadala wa Benzema na kwamba Kane ni lengo lao kuu baada ya nahodha huyo wa Tottenham Hotspur kuwa na kiwango bora.

Tayari uongozi wa Tottenham umeweka wazi kwamba hauna nia ya kumuuza Kane msimu huu licha ya ukweli amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake.

Kane pia ni chaguo la kwanza la uhamisho katika timu ya Manchester United msimu huu lakini Ofisa Mtendaji Mkuu wa Spurs Daniel Levy hana nia kufanya biashara na klabu yoyote ya Ligi Kuu England.

Ukweli huo unaweza kufungua mlango kwa Madrid, itategemea msimamo wa Kane kuhusu hatma yake na bado hajashinikiza kuondoka Spurs msimu huu.

Related Articles

Back to top button