K2ga afunguka sababu za wasanii kuondoka kwenye lebo

DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Karim Rashid, ‘K2ga’, amesema kuwa sababu kubwa inayowafanya wasanii wengi kuondoka kwenye lebo zao za muziki ni kutafuta ukuaji binafsi na kipato kikubwa.
K2ga amesema kuwa kila msanii anakumbana na changamoto tofauti akiwa ndani ya lebo, hali inayowasukuma baadhi yao kuchagua kujitegemea.
“Kila mtu ana changamoto zake akiwa kwenye kundi, kwa hiyo siwezi kusema changamoto halisi ni ipi, lakini nahisi kila mtu anatamani kuwa mkubwa zaidi na kupata pesa,” amesema K2ga.
Awali, K2ga alikuwa chini ya lebo ya Kings Music, inayomilikiwa na msanii Alikiba, lakini kwa sasa ametangaza rasmi kuwa hayupo tena chini ya lebo hiyo.
Msanii huyo amesema kuwa kwa sasa amechagua kujitegemea katika shughuli zake zote za muziki, akiamini kuwa hatua hiyo itamsaidia kukuza kipaji chake na kusimamia kazi zake kwa uhuru zaidi.
“Mimi sipo Kings kwa sasa, hivi sasa ni msanii ninayejitegemea kwenye kazi zangu,” amesisitiza K2ga.
Hatua ya K2ga inaongeza idadi ya wasanii wa Bongo Fleva wanaochagua kujitegemea baada ya kuondoka kwenye lebo kubwa, wakilenga maendeleo ya haraka na udhibiti wa moja kwa moja wa kazi zao.




