Jux: Priscy, ametimiza ndoto yangu

DAR ES SALAAM: MSANII nyota wa Bongo Fleva, Juma Mkambala maarufu kama Jux, ameandika ujumbe mzito wa mapenzi kupitia mitandao ya kijamii akimtaja mke wake Priscilla Ojo ‘Priscy’ kuwa ndiye sababu ya ndoto zake nyingi kutimia.
Ujumbe huo umeambatana na wimbo mpya aliouweka unaoitwa Thank you yaani Asante, akitoa shukrani kwa mwanamke huyo ambaye ameonekana kwa sasa ni mjamzito.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Jux amesema kuwa muziki kwake umekuwa lugha ya kuwasilisha hisia, na kwamba wimbo wake mpya unaelezea upendo wa dhati na shukrani kubwa kwa mpenzi wake.
“Kila ndoto niliyowahi kuishikilia kwa karibu sasa inatimia, yote hii ni kwa sababu nimepata mwenzi wa maisha. Muziki umekuwa lugha yangu ya hisia, na wimbo huu ni maelezo yangu ya ndani kabisa ya upendo na shukrani.” ameandika Jux.
Jux ameongeza kuwa wimbo huo ameutoa maalum kwa ajili ya familia yake na hasa kwa Priscy, ambaye amebadilisha kabisa maisha yake. Ameeleza pia kwamba amekuwa mwanaume mwenye furaha zaidi duniani, na hawezi kusubiri kuanzisha familia na kulea watoto wao pamoja.
“Ni wimbo maalum kwa familia yangu, kwa mwanamke aliyebadilisha dunia yangu. Priscy umenifanya kuwa mwanaume mwenye furaha zaidi duniani. Nakupenda sana, na siwezi kusubiri kulea watoto wetu wazuri pamoja,”alisema.
Mwisho