Joao Pedro atuma salamu nzito EPL

EAST RUTHERFORD, Mshambuliaji mpya wa Chelsea Joao Pedro alishindwa kushangilia baada ya kufunga mabao mawili na kuipeleka Chelsea katika fainali ya Kombe la Dunia la Klabu mabao ambayo yalizamisha jahazi la klabu yake ya zamani ya Fluminense katika mechi kali iliyochezwa kwenye Uwanja wa MetLife usiku wa kuamkia leo.
Mshambuliaji huyo wa Brazil mwenye miaka 23 ambaye ametua Chelsea kutoka Brighton & Hove Albion siku sita zilizopita, alifunga bao la kwanza dakika ya 18 kwa shuti zuri kabla ya kurudi tena kambani mapema kipindi cha pili na kuifungia timu yake bao la ushindi wa 2-0 na kutinga fainali kibabe.
Pedro Aliinua mikono juu kwa kuomba msamaha baada ya kila goli dhidi ya klabu ambayo alitumia miaka yake ya kujitafuta hata wachezaji wenzake wa Chelsea walipomzunguka kushangilia nae aliishia kutabasamu kwa muda mfupi tu.
“Klabu hii (Fluminense) walinipa kila nilichoncho. Walinifungulia Dunia. Ikiwa niko hapa kwa sababu waliniamini. Ninashukuru sana lakini huu ni mpira lazima niwe ‘professional’. Ninawasikitikia lakini lazima nifanye kazi yangu.” alisema Pedro kwenye mahojiano na DAZN baada ya mchezo huo
Pedro alicheza mechi yake ya kwanza katika mchezo wa robo fainali ya CWC dhidi ya Palmeiras Ijumaa iliyopita Chelsea ikishinda 2-1 w akiwa amefanya mazoezi machache tu na kikosi cha kwanza siku nne baadaye alikuwa kwenye kikosi kinachoanza.
Usajili wa Mbrazil huyo ni harakati za Chelsea kupunguza uhaba wa mshambuliaji kikosini hapo mwezi mmoja baada ya kumsajili ‘straika’ mwingine raia wa England Liam Delap. Chelsea itapambana na mshindi wa nusu fainali ya pili ya leu usiku kati ya Paris St Germain na Real Madrid katika Fainali itakayopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa MetLife.




