JKT Queens yaahidi Kombe CECAFA kufuzu Afrika

DAR ES SALAAM: MSEMAJI wa JKT Queens, Masau Bwire, amesema timu hiyo imejipanga vyema kwa safari ya kushiriki mashindano ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa upande wa wanawake na inalenga kuiletea heshima Tanzania.
Michuano hiyo ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) inatarajiwa kuchezwa nchini Kenya kuanzia Alhamisi ya Septemba 4, hadi 16, mwaka huu.
Akizungumza na SpotiLeo, Bwire alisema JKT Queens inatarajia kuanza kampeni zake kwa mechi muhimu dhidi ya JKU ya Zanzibar, itakayopigwa Ijumaa, na kwamba maandalizi yote yamekamilika.
“Tumejipanga kupigana kuhakikisha tunashinda na kuendelea mbele. Timu hii imebeba dhamana ya kupeperusha bendera ya Tanzania na tunataka kuonesha uwezo mkubwa ili kuleta heshima kwa taifa letu, Afrika Mashariki na bara zima la Afrika,” alisema Bwire.
Aliongeza kuwa kikosi cha JKT Queens kinaundwa na wachezaji wa Kitanzania pekee, jambo linaloongeza thamani na heshima ya nchi katika mashindano hayo.
“Wachezaji wetu wote ni wa Kitanzania, jambo linaloonesha kuwa tunacho kipaji cha ndani cha kuaminika. Tunaomba Watanzania wote watuunge mkono kwa maombi na moyo ili tufanikishe malengo yetu ya kulitwaa taji hili kubwa,” alisema.
JKT Queens imewahi kushiriki mashindano hayo na kupata uzoefu unaowapa matumaini ya kufanya vizuri zaidi msimu huu, huku lengo lao kuu likiwa ni kuifikisha Tanzania kileleni katika soka la wanawake barani.