Ibraah afunguka kuhusu tetesi za kujiunga na WCB

MSANII wa Bongo Fleva, Ibraah, ameweka wazi msimamo wake kuhusu tetesi za kujiunga na lebo ya WCB Wasafi inayomilikiwa na Diamond Platnumz.
Akizungumza nchini Kenya, Ibraah, maarufu pia kama Chinga, amesema kuwa kama kuna mpango wowote unaoendelea kuhusu yeye kuhamia WCB, basi mashabiki watakuwa wa kwanza kujua.
“Kama kuna chochote kinaendelea basi mtakiona, kwasababu hakuna kitakachojificha. Ni kazi na tunapofanya kazi siku zote tunahitaji umoja, kwahiyo kama itatokea mtaona, hatutoficha chochote,” amesema Ibraah.
Ameongeza kuwa kwa sasa bado yupo chini ya lebo ya Oya Gang, lakini akasisitiza kuwa hatakuwa na sababu ya kuficha endapo ataamua kufanya kazi na WCB Wasafi.
“Siwezi kuficha chochote kama WCB Wasafi ndio sehemu nitakayoenda, mtaona kwasababu ndio nitakuwa nafanya nao kazi. Lakini kwa sasa tupo Oya Gang,” alisisitiza msanii huyo.
Kauli hiyo imekuja kufuatia uvumi uliosambaa mtandaoni ukidai kuwa huenda Ibraah akajiunga na lebo hiyo kubwa Afrika Mashariki.