Africa

Ibenge: Tunahitaji umakini michezo ijayo

DAR ES SALAAM- KOCHA Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge, amesisitiza haja ya wachezaji wake kuongeza umakini wa kiuchezaji, uimara wa kisaikolojia na matumizi sahihi ya nafasi katika michezo ijayo, akisema timu yake bado ina nafasi ya kufanya vizuri zaidi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Ibenge amesema pamoja na ushindi walioupata katika mchezo uliopita dhidi ya Nairobi United, bado kuna mapungufu yanayohitaji kurekebishwa ili Azam FC iendelee kubaki kwenye ushindani, akibainisha kuwa akili ya kiufundi na ujasiri wa kushambulia ni mambo muhimu yanayopaswa kuimarishwa.

Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya mchezo huo, kocha huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alisema ushindi huo umeipa Azam FC uhai mkubwa katika kundi, huku akieleza kuwa pointi tatu walizopata zimewaweka kwenye nafasi nzuri ya kuendelea kupambana.

“Tulihitaji sana pointi tatu. Wapinzani Wydadn na Maniema wanaongoza kwa pointi tisa, lakini sisi sasa tuna pointi sita, jambo linalotuweka bado hai kwenye mashindano,” alisema Ibenge.

Hata hivyo, alikiri kuwa mchezo huo haukuwa mwepesi, akieleza kuwa kisaikolojia wachezaji wake hawakuwa kwenye hali bora, hali iliyosababisha kushuka kwa kiwango cha utekelezaji wa mbinu walizojiwekea.

Ibenge alisema baada ya kufunga bao la mapema, wachezaji wake walicheza kwa tahadhari kupita kiasi na kushindwa kufuata maelekezo ya benchi la ufundi, jambo lililoathiri kasi na ubunifu wa ushambuliaji.

Mchezo ujao Azam FC inatarajia kucheza na AS Maniema nyumbani kwenye Uwanja wa New Amaan Zanzibar hivyo, wanahitaji kushinda mchezo huo kwa mabao kuanzia matatu kujiweka katika nafasi nzuri.

Related Articles

Back to top button