Hata Salah asingeweza :Postecoglou

LONDON:MENEJA wa Tottenham Hotspur Ange Postecoglou amesema kwa jinsi kikosi chake kinavyotengeneza nafasi chache, hata angekuwa na mshambuliaji wa Liverpool Mohammed Salah bado angekuwa na wakati mgumu kufunga mabao katika klabu hiyo ya London.
Licha ya kukiri kuwa Salah ni mchezaji bora kwa sasa Postecoglou amesema asingeweza kufanya anayofanya Liverpool kwa kuwa kikosi chake hicho hakitengenezi nafasi kwa mshambuliaji wa aina yake.
“Mo ni mchezaji wa kiwango cha hali ya juu sana kwa sasa, sina shaka na hilo. Lakini ukimuweka kwenye kikosi chetu hivi sasa angekuwa sawa na sisi tu, angepata tabu kufunga kwa sababu ni hali tunayopitia kama timu” kocha huyo alisema kwenye mkutano na wanahabari.
“Unahitaji timu iliyo kwenye kiwango kizuri, inayotengeneza nafasi na inayocheza vizuri mbele na kuwa na msingi mzuri wa ulinzi. Sisi hatuna chochote kati ya hivyo kwa sasa, tunategemea jitihada binafsi” Aliongeza.
Salah amewaka msimu huu akiwa na mabao 21 na ‘asisti’ 17 katika mashindano yote msimu huu
Spurs wapo katika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi kuu ya England watakutana na Liverpool ambao ni vinara katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Kombe la Carabao usiku wa leo.